MBUNGE wa Jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akitoa maelekezo kwa Diwani wa kata ya Mwasubuya Sylvester Chenge (katikati) katika mkutano wwa kuwasilisha Ilani ya CCM 2020/2025.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MBUNGE wa Jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo Mathew ameipongeza serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha Huduma ya Umeme katika vijiji 84 vya Jimbo hilo ndani ya miaka mitano.
Aidha, amesema kuwa huduma hiyo ya Umeme ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025, na kwamba katika bajeti ijayo ya 2025/2026 serikali itafikisha umeme kwenye vitongoji.
Mhandisi Kundo ameyasema hayo leo, kwenye Mkutano maalumu uliofanyika kata ya Mwasubuya kwa ajili ya kuwasilisha Ilani ya CCM 2020/2025, na ameeleza kuwa kwa miaka mitano (2015/2020), kata hiyo ilipatiwa shilingi Mil. 230 na awamu ya Dk. Samia 2020/2025 serikali imetoa Shilingi Bil. 1.4 kwa ajili ya miradi ya Maendeleo.
Mhandisi Kundo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, amesema kuwa kuanzia bajeti ijayo ya 2025/26, serikali ya Rais Dk. Samia inakwenda kupenya na kufikisha umeme kwenye vitongoji.
"mmetuamini na kutuheshimisha kwa miaka mitano, tumepelekea Umeme kwenye vijiji vyote vya Jimbo la Bariadi...katika bajeti ijayo tutafikisha umeme kwenye vitongoji" amesema Mhandisi Kundo na kuongeza.
"Hongereni kwa kuiamini serikali ya CCM,
Vijiji vyote 84 ndani ya Jimbo la Bariadi vimefikiwa na Umeme...lengo letu limefanikiwa, natumia fursa hii kumshukuru Rais Dk.. Samia kutupatia huduma ya umeme".
Mbunge huyo amewapongeza wananchi kwa kuchagua viongozi wanaotokana na CCM ambao waliahidi kutekeleza ilani ya CCM na kusimamia miradi ya maendeleo.
Amesema katika kata ya Mwasubuya, serikali imetoa kiasi cha shilingi Mil. 630 ili kutekeleza mradi wa maji ambao umekamilika na unatoa maji.
Katika sekta ya Mawasiliano, Mbunge huyo amesema serikali imejenga Minara 42 kwa ajili ya kuboresha huduma ya mawasiliano katika Jimbo la Bariadi.
Amesema watahakikisha wanaendelea kunaimarisha mawasiliano sababu ni njia ya pili ya kukuza uchumi wa taifa na mwananchi mmojammoja.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo amekabidhi mipira minne na pea Moja ya jezi kwa kila Kijiji katika vijiji vya Igabulilo, Isengwa, Miswaki na Mwasubuya wakati huo kata ya Mwasubuya ikiabidhiwa mipira mitatu na pea Moja ya jezi.
Pia, Mhandisi Kundo amekabidhi pampu nne za maji kwa ajili ya vijiji vya kata hiyo ambapo Kila kijiji kitapatiwa pampu moja ambazo zimetolewa na Rais Dk. Samia ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma ya maji.
Mwisho.
0 Comments