Na Matukio Daima App.
MBEYA.Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeungana na wadau wengine kutoa salamu za pole kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa katika ajali ya gari mkoani Mbeya.
Ajali hiyo, imetokea usiku wa Jumamosi Juni 7, 2025 katika eneo la Mlima Iwambi, mkoani Mbeya na kusababisha vifo vya watu 28 huku wengine wanane wakijeruhiwa.
Taarifa ya Chadema iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, iliyotolewa jana Jumapili Juni 8, 2025 imeeleza kusikitishwa na ajali hiyo.
"Tunatambua majonzi, huzuni na mshtuko mkubwa mlionao katika kipindi hiki kigumu. Tunawaombea faraja, subira na nguvu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili muweze kuvumilia machungu ya msiba huu mkubwa," imeeleza.
Imeeleza Chadema inaungana na wote kwa moyo wa maombolezo na kuwapa pole kwa msiba huo uliotikisa Taifa.
Aidha, chama hicho, kimewatakia majeruhi wote uponaji wa haraka na kuimraika afya zao.
Naye, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Ifisi, Dk Morice Martin alisema kati ya watu 28 waliofariki dunia, mmoja pekee ndiyo alifariki wakati anaendelea na matibabu na wengine wote walifikishwa wakiwa wamefariki.
Baadhi ya majina waliofariki dunia ni, Furaha Gabriel, Josephine Hagai, Joseph Hagai, Odfen Simon, Lydia Gambi, Aman Daud, Mecia Zabron, Edna Mwangomita na Derick Ndanya wote wakazi wa Mbalizi mkoani Mbeya.
Wengine waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Elisiana Mwsifu, Narice Mwasifu wakazi wa Mbabu na Juma Ramadhan, Deborah Wilson, Gwekelo Zakaria na Lawrence Semwanza wakazi wa Mbalizi.
0 Comments