Kufuatia changamoto ya ubovu wa barabara inayowakabili wananchi wa kata za Shizuvi na Ilembo tarafa ya Isangati Jimbo la Mbeya vijijini hasa katika kusafirisha mazao na bidhaa mbalimbali, Serikali imesaini mikataba miwili na wakandarasi kwa ajili ya kujenga barabara kwa kiwango cha Changarawe ikiwemo barabara ya Sapanda Isonso Ilembo.
Wananchi wa kata hizo huenda wakaondokana na changamoto hiyo kutokana na mpango wa Serikali kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha Changarawe kama ilivyoelezwa na meneja wa wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) mkoa wa Mbeya Mhandisi Alberto Kindole kuwa barabara hizo zitagharimu zaidi ya shilingi billion mbili.
Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi wa kata za Shizuvi na Ilembo kwenye shughuli ya utiaji saini na wakandarasi, meneja huyo wa TARURA mkoa wa Mbeya ameeleza kuwa barabara za vijijini ni muhimu na zinasaidia katika usafirishaji hasa wa mazao mbalimbali kama ilivyoombwa na Mbunge wa Mbeya vijijini na madiwani kwa nyakati tofauti.
Akizungumza na wananchi hao, Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza, amesema wananchi wake wana uhitaji mkubwa wa barabara utakaowasaidia katika usafirishaji mazao na wagonjwa ikizingatiwa kuwa eneo hilo ni wazalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo Mbao, Pareto na viazi.
Pamoja na hayo Mbunge Njeza ameishukuru Serikali kwa uidhinishaji fedha zaidi ya shilingi billion mbili na kwa ajili ya barabara mbili
Barabara zilizosainiwa mikataba yake kwa ajili ya kuanza ujenzi ni za Ilembo Mwala na ile ya Sapanda Ilembo Isonso ambazo zote zitaanza ujenzi wake rasmi mwanzoni mwa mwezi Juni 2025 na zitajengwa kwa kiwango cha Changarawe kwa muda wa miezi nane.
0 Comments