Serikali imesema haitosita kumchukulia hatua mzalishaji au msambazaji wa bidhaa yeyote atakayezalisha u kusambaza bidhaa feki ikiwemo kuingiza nchini kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa kanda wa Tume ya Ushindani (FCC) nyanda za juu kusini Dickson Mbanga ambaye amesema vitendo vya kuuza na kusambaza bidhaa bandia vinadhoofisha ustawi wa taifa na jamii kwa ujumla, hivyo serikali kupitia FCC haiwezi kuvifumbia macho.
Katika hatua nyingine, Mbanga ametoa wito kwa wananchi kujitokeza katika ofisi za FCC za kanda kupata elimu ya namna ya kutambua bidhaa bandia.huku akisema kuwa tume inaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuwajengea uwezo wa kujilinda dhidi ya bidhaa zisizo halali.
Kwa upande wake, Andason Luiza, Mkaguzi na Afisa Mdhibiti wa FCC, amesema kuwa sheria zipo wazi kwa mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na biashara au usambazaji wa bidhaa bandia. Ameeleza kuwa adhabu kwa makosa hayo ni pamoja na kutozwa faini, kufikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua kulingana na uzito wa mzigo aliokutwa nao, ikiwemo kulipia gharama za kuteketeza bidhaa hizo.
FCC imesisitiza kuwa mapambano dhidi ya bidhaa bandia ni jukumu la kila mmoja, hivyo ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kulinda afya, usalama na uchumi wa taifa.
0 Comments