Header Ads Widget

WANANCHI KAHE MASHARIKI WAMKABIDHI NDAFU MBUNGE DKT. KIMEI KWA UTENDAJI BORA



Na WILLIUM PAUL, VUNJO. 


WANANCHI wa Kata ya Kahe Mashariki Jimbo la Vunjo wilayani Moshi wakiongozwa na wazee  wamempongeza Mbunge wa Jimbo hilo Dkt. Charles Stephen Kimei kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi cha mwaka 2020 - 2025, kwa kumzawadia ndafu (mbuzi dume) kama ishara ya heshima na shukrani.


Wakizungumza jana wakati wa hafla hiyo, wazee wa kata hiyo wakiongozwa na Silas Msumanje, Solomon Kimati na Rasuli Kitia walieleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Dkt. Kimei kupitia serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni makubwa. 



Walitaja mafanikio hayo kuwa ni Ujenzi wa zahanati katika vijiji vya Kochakindo na Ghona, ujenzi wa jengo la afya ya uzazi, mama na mtoto katika zahanati ya Kyomu na ushawishi uliofanikisha upatikanaji wa shilingi bilioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chekereni - Kahe - Mabogini. 


Mafanikio mengine ni ushawishi wa serikali kulijenga bwawa la Urenga kwa ajili ya huduma ya maji na kilimo. 



Wazee hao walimpongeza Dkt. Kimei kwa uongozi wake wa karibu na wananchi na kumtaka kuchukua tena fomu ya kugombea ubunge kwa kipindi kingine, huku wakiahidi kumuunga mkono kwa dhati.


Kwa upande wake, Dkt. Kimei aliwashukuru wananchi na jamii ya Kahe Mashariki kwa kuwa mstari wa mbele katika maendeleo na kuahidi kuendelea kuwa mwakilishi mwaminifu, mchapakazi na mwenye kusikiliza wananchi wake.


"Nawashukuru kwa moyo huu wa upendo na mshikamano tumefanya mengi kwa pamoja, na bado safari ya maendeleo inaendelea nipo pamoja nanyi," alisema Dkt. Kimei.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI