Header Ads Widget

"WAGANGA WALAZIMISHA NGONO NA KUWAREKODI PICHA CHAFU WAKE ZA WATU"

Na Matukio Daima App

GEITA; JESHI la Polisi mkoani Geita limebaini baadhi ya waganga wa kienyeji na tiba mbadala wanatumia nafasi zao kufanya matukio ya udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake kwa kisingizio cha matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Safia Jongo amesema hayo katika mkutano wa hadhara Kijiji cha Nyakagomba wilayani Geita.

Amesema uchanguzi umebaini baadhi ya waganga wa tiba asili wanawalazimisha wateja wao wa kike kufanya nao mapenzi na kisha kuwarekodi picha chafu kama kitisho iwapo watatoa siri.

"Tutibu watu kulingana na vile mababu walituelekeza, sasa hivi imeingia tabia mbaya zaidi kwenu nyie waganga mnafanya zinaa na wake za watu kwa kuwadanganya mnawatibia.

"Mbaya zaidi mnaenda mbali mnawarekodi akitaka kukuacha unamtishia nitakuua, unaanza kumrushia zile picha ulizomrekodi na kumtishia kwamba utamdhalilisha," amesema Kamanda Jongo.

 Aidha Kamanda Jongo, amewaonya baadhi ya waganga wa tiba asili wenye tabia ya kupandikiza chuki na kutumia ramli chonganishi kwa wanasiasa.

Amesema baadhi ya waganga hao wamekuwa wakiwadanganya wagombea wakati wa uchaguzi na kusababisha matukio ya ukatili nyakati za uchaguzi.

"Changamoto kubwa tuliyonayo mnawadanganya sana wagombea nyie waganga, acheni, kutumia hizo mbinu kuwaharibu viongozi wetu, na hatimaye mnatusababishia uhalifu," amesema.

MWISHO.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI