Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema vita nchini Ukraine "havitamalizika hivi karibuni", katika mahojiano na Fox News.
Vance alisema swali linalokabili utawala wa Marekani kwa sasa ni jinsi gani inaweza kusaidia Urusi na Ukraine "kupata muafaka" ili kumaliza mzozo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Lakini, Vance aliongeza, "itakuwa juu ya [Urusi na Ukraine] kuafikiana makubaliano ya kukomesha mzozo huu wa kikatili.
Maoni yake yanakuja muda mfupi baada ya Marekani kutia saini mkataba wa madini adimu ya Ukraine kama mabadilishano ya malipo ya usaidizi wa usalama wa Marekani siku zijazo.
Vance alitoa maoni hayo katika mahojiano ya wigo mpana, ambapo alitetea mtazamo wa Trump kuhusu vita vya Ukraine.
"Ndio, bila shaka, [Waukraine] wana hasira kwamba walivamiwa," Vance aliongeza. "Lakini je, tutaendelea kupoteza maelfu na maelfu ya wanajeshi kwa umbali wa maili chache za eneo hili au lile hadi lini?"
Trump wiki hii alipendekeza kuwa Ukraine inaweza kuwa tayari kuachia Crimea - ambayo Urusi iliivamia mwaka 2014 - ili kufikia suluhu la mapatano.
Lakini Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alikuwa amedokeza hapo awali kwamba hangeweza kukubali udhibiti wa Urusi katika rasi hiyo, akitoa mfano wa katiba ya Ukraine .
Katika mahojiano tofauti na Fox News siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema kuna haja ya kuwa na "mafanikio" katika mzozo wa hivi karibuni, vinginevyo Trump "atalazimika kuamua ni muda gani atajitolea kumaliza mzozo huu".
Rais wa Urusi Vladimir Putin wiki hii alitangaza usitishaji vita wa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 8 Mei, ili kuendana na sherehe za kumbukumbu ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.
0 Comments