NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Iringa Mjini, Islam Huwel, ametoa wito kwa wana-CCM na Watanzania kwa ujumla kutoruhusu wapinzani wa kisiasa kuipotosha jamii kuhusu kazi na mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amewataka wote wanaoamini katika maendeleo kujibu upotoshaji huo kwa hoja na vielelezo vya miradi halisi ya maendeleo.
Islam Huwel alitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza kwenye kipindi cha Tanzania ya Leo kinachorushwa na Matukio Daima TV, Katika mahojiano hayo, Huwel alieleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu, maji na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, hatua ambazo ni dhahiri kuwa zinaletwa na uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia.
“Leo hii tunaona shule mpya zikijengwa kila kata, mabweni yakiimarishwa, watoto wa kike wakipewa kipaumbele na ada zinalipwa na serikali. Hii ni hatua kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo wazazi waliteseka sana kugharamia elimu ya watoto wao.
Hatuwezi kuruhusu watu waliokataa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu waje kupotosha ukweli huu wa maendeleo,” alisema Huwel kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika kuboresha maisha ya Watanzania kupitia miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ununuzi wa ndege, maboresho ya hospitali za rufaa na vituo vya afya, pamoja na mpango wa kuwainua wanawake na vijana kupitia mikopo ya halmashauri isiyo na riba.
Islamu Huwel alisisitiza kuwa, kama wana-CCM, kuna wajibu wa kutetea na kueleza kazi zinazofanywa na serikali kwa kutumia takwimu na ushahidi wa maendeleo. Alisema chama cha mapinduzi hakiwezi kuruhusu nafasi ya watu kueneza taarifa za uongo ilhali wananchi mashuhuda wa mabadiliko wanayaona kwa macho na kuyahisi kwenye maisha yao ya kila siku.
“Nasisitiza tena, tutumie mitandao ya kijamii, majukwaa ya kijamii na kila fursa kuelezea kazi zinazofanywa na serikali yetu. Huu si wakati wa kulalamika kimya kimya tunapokuwa tunaona watu wakidhalilisha juhudi za serikali. Ni wajibu wetu kupinga kwa hoja,” alisema.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano, Huwel aliipongeza Serikali ya Rais Samia kwa kuwa na maono ya wazi katika diplomasia ya uchumi, hatua ambayo imefungua milango kwa wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi kuja Tanzania. Alisema kupitia mikutano ya kimataifa, mikataba ya biashara, na ziara za kitaifa, Rais Samia ameipa Tanzania sura mpya ya kimataifa na heshima katika jukwaa la dunia.
Aidha, Huwel aliwahimiza vijana kutumia nafasi ya amani na utulivu uliopo nchini kujijengea maisha bora kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali. Alieleza kuwa siasa safi lazima ziende sambamba na maendeleo, na kwamba vijana wa CCM wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha mijadala ya maendeleo na siyo matusi na propaganda zisizo na tija.
“Chama Cha Mapinduzi kinaongozwa na sera zinazotegemea ushahidi wa utekelezaji. Tunapopata nafasi kama hii, hatuna budi kuziambia jamii kuwa Dkt. Samia ni kiongozi anayeona mbali. Tumpe ushirikiano na tulinde heshima ya taifa letu kwa kuonesha kazi badala ya kulumbana na watu wanaotafuta umaarufu wa kisiasa,” aliongeza.
0 Comments