Header Ads Widget

RAS SONGWE ATAKA UWAJIBIKAJI KATIKA USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO TUNDUMA.

 


Na Moses Ng’wat, Tunduma.

Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda, amewataka watumishi wa umma wanaosimamia miradi ya maendeleo kuhakikisha wanatunza nyaraka na vielelezo vyote muhimu hasa wakati wa ukaguzi ili kuepusha sintofahamu.


Seneda alitoa agizo hilo Mei 19, 2025, wakati wa ziara ya siku moja ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, ambapo alibaini changamoto kadhaa ikiwemo kukosekana kwa nyaraka muhimu na mpango kazi wa baadhi ya miradi.



“Mara nyingi tumewaambia lazima tuwe na utaratibu wa kutunza nyaraka zote zinazohusiana na miradi, kwani tunapokuja kukagua na kukosa nyaraka hizi  kunazua maswali mengi  na kunaashiria uzembe,” alisema RAS Seneda.


Hata hivyo  akiwa katika eneo la mradi wa ujenzi wa jengo la Wodi na Upasuaji (Block B) katika Hospitali ya Mji wa Tunduma, mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 2.3, hakuweza kuukagua kutokana na ukosefu wa nyaraka muhimu.


Katika ziara hiyo, alitembelea pia mradi wa ujenzi wa nyumba ya kupumzikia wageni (Rest House) na mgahawa katika eneo la maegesho ya magari ya mizigo mpakani mwa Tanzania na Zambia, unaogharimu zaidi ya Shilingi milioni 600.


Hata hivyo, alionyesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji, akisema kuwa kuchelewa kwa mradi huo tangu uanze Februari 2022 ambao hadi sasa haujakamilika hadi sasa licha ya kutakiwa kukamilika tangu mwaka 2023 ni dalili ya uzembe.


Ofisa Mipango wa Halmashauri, Innocent Maduhu, aliomba muda zaidi ili kumalizia kazi zilizobaki kwa kuwa fedha zimeshatengwa, lakini ombi hilo halikukubaliwa na RAS Seneda ambaye alisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuchelewesha miradi ya maendeleo inayogharimu fedha za umma.

Katika hatua nyingine, Seneda alitembelea ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri katika eneo la Chapwa, linalotekelezwa kwa njia ya Force Account, ambapo alikuta mafundi hawapo kazini licha ya taarifa kuonyesha kazi inaendelea.

Kutokana na kasoro hizo, Seneda alitoa siku 15 kwa watendaji hao wa Halmashauri kuhakikisha kasoro zote zinatekelezwa na miradi hiyo kukamilika kabla ya ziara nyingine atakayofanya Juni 6, 2025.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI