NA HAMIDA RAMADHANI – MATUKIO DAIMA APP, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita yametokana na utekelezaji wa matakwa ya maendeleo na ustawi wa wananchi kama yalivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 hadi 2025.
Rais Samia ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma, mara baada ya kupokea tuzo maalum ya heshima iliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua uongozi wake mahiri ulioelekezwa katika kuleta maendeleo jumuishi na ustawi wa taifa.
Akitoa shukrani zake, Rais Samia amesema tuzo hiyo ni ushahidi wa kuthamini kazi ya pamoja kati ya mihimili ya dola, viongozi wa serikali, na wananchi waliotoa ushirikiano wa karibu katika kipindi cha uongozi wa awamu ya sita na kuwezesha nchi kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Aidha, amelitaka Bunge kuendelea kusimamia vyema majukumu yake kwa kushirikiana na serikali kupitia mijadala, kupitisha sheria muhimu, na kutoa ushauri wa kitaalamu unaoleta tija kwa taifa. Rais Samia amewapongeza pia wabunge kwa namna wanavyotetea maslahi ya wananchi ndani na nje ya Bunge.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, amempongeza Rais Samia kwa uongozi wake wa kipekee, akibainisha kuwa tuzo hiyo imetolewa kwa niaba ya wabunge wote kama ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Amesema kupitia uongozi wa Rais Samia, taifa limeshuhudia mageuzi makubwa katika kuimarisha Muungano, utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, pamoja na maendeleo katika sekta za elimu, afya, madini, utalii, uchukuzi, kilimo, nishati na diplomasia ya kimataifa.
Aidha, Spika ameeleza kuwa falsafa ya uongozi wa Rais Samia inayojulikana kama R4, ambayo inajumuisha maridhiano, ustahimilivu wa jamii na taifa kukabiliana na changamoto, mageuzi ya kisera, na ujenzi wa mifumo mipya ya kiutendaji, imekuwa dira ya mafanikio ya serikali ya awamu ya sita.
Kupitia usimamizi wa serikali hiyo, hoja kumi na tano za Muungano zimepatiwa ufumbuzi, jengo la kitegauchumi limezinduliwa Kaskazini Unguja, na ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar umeimarika kupitia wizara, idara na taasisi mbalimbali.
Sekta ya elimu imeendelea kuboreshwa kwa kupanua miundombinu, kuongeza bajeti na kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Serikali pia imeendelea kusukuma mbele ajenda ya maendeleo kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa na kukuza ushirikiano wa kimataifa.
Kwa ujumla, hotuba ya Rais Samia imesisitiza mshikamano wa kitaifa, dhamira ya maendeleo jumuishi, na maono ya kujenga Tanzania yenye usawa, mshikamano na mafanikio kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
0 Comments