Serikali ya Tanzania imeonya juu ya ongezeko la matukio ya upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii, kufuatia taarifa potofu zilizochapishwa kwenye akaunti zinazodaiwa kuwa za taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Jeshi la Polisi Tanzania limetoa taarifa rasmi likikanusha kuhusika na taarifa zilizosambazwa kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), zikidaiwa kuwa zimetoka katika akaunti yao.
Inaelezwa kuwa watu wasiofahamika kuingia kwenye akaunti ya Jeshi hilo na kuanza kuchapisha taarifa mbalimbali ambazo Jeshi hilo limekanusha kuhusika nazo.
Taarifa ya Jeshi hilo imesema taarifa zilizochapishwa ni za uongo, zisizo na maadili, na zina lengo la kupotosha umma. Jeshi hilo limeeleza kuwa halijaandaa wala kusambaza taarifa hizo, na tayari linaendelea kuwatafuta watu waliotengeneza na kuzisambaza ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Sambamba na hilo, taarifa ya Katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji mkuu wa Serikali, imethibitisha kuwepo kwa ongezeko la akaunti feki zinazofanana kwa jina na zile halali za taasisi.
Akaunti hizo zimetajwa kuwa zimekuwa zikitumika kuchapisha taarifa za upotoshaji zenye nia ya kuzua taharuki kwa wananchi.
Mbali na Jeshi la Polisi, mitandao mingine inayodaiwa kuwa imeathirika na matukio hayo ni pamoja na Tanzania Investment Center (TIC), huku mitandao ya Airtel Tanzania na klabu ya Simba SC ikitajwa pia, ingawa taarifa hizo bado hazijathibitishwa rasmi na mamlaka husika zinazomiliki mitandano tajwa.
Serikali imewahimiza wananchi kuwa makini na taarifa wanazozipata mtandaoni, na kuwataka kujiridhisha kwa kufuatilia akaunti rasmi za taasisi au kuwasiliana na mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zozote.
"Tunatoa onyo kwa wote wanaofanya uhalifu huu. Hatua kali za kisheria zinachukuliwa," amesema Gerson Msigwa, Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali.
0 Comments