Header Ads Widget

NCAA YAENDESHA OPARESHENI YA KUTOKOMEZA MAGUGU KAROTI NDANI YA ENEO LA HIFADHI.

Na,Jusline Marco;Arusha

Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) imeendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi wa vijiji vinavyopakakana na hifadhi ya Ngorongoro kupambana na mmea vamizi na hatari wa Gugu Karoti ambao umeota katika baadhi ya maeneo ili kuhakikisha mazingira ya hifadhi na shoroba za wanyamapori yanabaki salama kwa uhifadhi endelevu.

Hatua ya ushirikishaji wa jamii ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kudhibiti mimea vamizi nchini, hususani katika maeneo ya yaliyohifadhiwa na kuzilinda shoroba muhimu zinazounganisha mifumo ya ikolojia kama vile shoroba ya Upper Kitete inayounganisha hifadhi za Ngorongoro, ziwa Manyara na Tarangire.

Afisa Uhifadhi darala la Kwanza Gregory Mtega kutoka NCAA  akiongoza wananchi wa Kijiji cha Upper Kitete na baadhi ya wataalam katika Oparesheni ya kung'oa magugu Karoti ameeleza kuwa  operesheni hiyo imefanyika kwa mafanikio makubwa kupitia ushirikiano kati ya NCAA, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu na shirika la PAMS na kuongeza kuwa juhudi hizo zinaendelea katika vijiji vingine vinavyopakana na hifadhi kwa ajili ya kuhifadhi uoto wa asili, malisho ya mifugo, na maisha ya wanyamapori.

Mtega ameongeza kuwa Gugu Karoti ni mmea unaosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kuwa unazaliana kwa kasi na ni tishio kwa wanyamapori, mifugo, na hata kilimo cha wananchi hivyo mamlaka hiyo imewekeza juhudi za kutosha kukabiliana nalo kwa kutumia njia mbalimbali.

Naye Afisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Kornelio Lengai, amepongeza ushirikiano wa NCAA na kueleza kuwa mmea huo umekuwa kikwazo kwa uzalishaji wa chakula na maisha ya wakazi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hivyo Jitihada za NCAA kushirikiana na wadau mbalimbali ni ishara nzuri katika uhifadhi endelevu kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Emanuel Siriri, mkazi wa kijiji cha Upper Kitete, ameishukuru NCAA kwa kuendelea kutoa elimu na kuwashirikisha wananchi wa kijiji hicho ambapo jitihada hizo si tu zinaleta matumaini bali zimefungua fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia kazi za udhibiti wa mmea huo ambao unapodhibitiwa unaboresha shughuli za kilimo na kupata mazao ya kutosha.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI