Mtandao wa X zamani Twitter umeminywa nchini Tanzania baada ya baadhi ya akaunti za taasisi za serikali na mashirika binafsi kudukuliwa na watu wasiojulikana.
Taasisi ya NetBlocks ambayo inafuatilia uhuru wa upatikanaji wa huduma za intaneti duniani iliripoti jana Jumanne usiku kuwa mtandao wa X umeminywa na mpaka leo asubuhi watumiaji wa mtandao huo nchini humo walikuwa hawawezi kujiunga nao.
Serikali ya Tanzania haijatoa tamko lolote juu ya kuminywa kwa mtandao wa X japo hapo awali walitoa onyo la kuwashughulikia waliofanya udukuzi wa akaunti za X nchini humo.
Akaunti ambazo zilidukuliwa hiyo jana ni za Jeshi la Polisi, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na shirika binafsi la mtandao was imu la Airtel Tanzania. Polisi na TIC wamefanikiwa kurejesha akaunti zao lakini Airtel Tanzania bado wamedukuliwa mpaka asubuhi ya leo Jumatao.
Wadukuzi hao awali walichapisha maudhui machafu ya ngono na baadae kutoa taarifa za uzushi kuwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefariki dunia.
Mara baada ya kufuta maudhui hayo, Polisi ilitoa taarifa rasmi ikikanusha kuhusika na taarifa zilizosambazwa kupitia mtandao wa X katika akaunti yao.
Katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa naye alitoa taarifa ya kuonya umma juu ya uwepo wa ongezeko la akaunti feki zinazofanana kwa jina na zile za taasisi halali.
Serikali imewahimiza wananchi kuwa makini na taarifa wanazozipata mtandaoni, na kuwataka kujiridhisha kwa kufuatilia akaunti rasmi za taasisi au kuwasiliana na mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zozote.
"Tunatoa onyo kwa wote wanaofanya uhalifu huu. Hatua kali za kisheria zinachukuliwa," amesema Msigwa.
0 Comments