Header Ads Widget

MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA LAMI IRINGA – KILOLO UNAVYOMHESHIMISHA MBUNGE JUSTINE NYAMOGA

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA 

Katika miaka ya hivi karibuni, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa imejipatia heshima kubwa kitaifa kutokana na maendeleo makubwa ya miundombinu, hasa kupitia ujenzi wa barabara ya lami inayounganisha Iringa Mjini na Kilolo. 


Mradi huu mkubwa umeendelea kuibua matumaini mapya kwa wananchi wa Kilolo mkoani Iringa , huku ukimuimarisha kisiasa Mbunge wa Jimbo hilo,  Justine Nyamoga, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.

Ujenzi wa barabara ya Iringa – Kilolo si tu kwamba unaunganisha maeneo ya vijijini na mijini kwa urahisi zaidi, bali pia umefungua fursa kubwa za kiuchumi kwa wakazi wa Kilolo. 

Wilaya ya Kilolo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kama vile mahindi, viazi, ndizi, maharage pamoja na bidhaa kutoka katika sekta ya misitu, hasa mbao.

 Kwa muda mrefu, changamoto ya barabara mbovu ilikuwa kikwazo kikubwa kwa wakulima na wafanyabiashara kufikisha bidhaa sokoni kwa wakati. 

Hivyo, mradi huu wa barabara ya lami umekuwa ukionekana kama mkombozi wa kweli kwa uchumi wa wakazi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa Justine Nyamoga, mafanikio haya makubwa yanatokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. 


Akizungumza na Matukio Daima Media, Nyamoga alieleza kuwa Rais Samia ameonesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha kuwa kila mwananchi ananufaika na matunda ya uhuru na maendeleo. 

“Huu ni ushahidi wa wazi kuwa serikali ya CCM ipo kazini na kwamba ahadi zinazotolewa wakati wa kampeni si maneno matupu, bali zinatekelezwa kwa vitendo,” alisema mbunge huyo.

Barabara ya Iringa - Kilolo yenye urefu wa kilomita 33 inajengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 63. 

Kazi hiyo kubwa ya ujenzi wa lami inaendelea kwa kasi, na tayari mafanikio makubwa yameanza kuonekana. 

Kupitia msukumo na ushawishi wa Mbunge Nyamoga, barabara nyingine ya Bomalang’ombe – Kidabaga – Ng’ang’ange – Mwatasi yenye urefu wa kilomita 26 imekarabatiwa kwa kiwango cha lami, na zaidi ya hapo, kilomita tisa zimeongezwa katika eneo hilo, jambo linaloongeza mtandao wa barabara za lami wilayani Kilolo.


Takwimu zinaonesha kuwa tangu nchi ipate uhuru, Wilaya ya Kilolo ilikuwa na jumla ya kilomita 9 pekee za barabara za lami. 

Hata hivyo, katika kipindi cha miaka mitano tu ya uongozi wa  Nyamoga kama Mbunge, zaidi ya kilomita 68 za barabara ya lami zimejengwa. 

Ongezeko hili la kilomita 59 linaashiria mapinduzi makubwa ya kiinfrastruktura katika eneo hilo.

 Wananchi wa Kilolo wana kila sababu ya kumpongeza mbunge wao na serikali kwa kushirikiana kuhakikisha maendeleo yanawafikia.

Faida za barabara hizi kwa uchumi wa Kilolo haziishii kwenye usafirishaji wa mazao pekee. 

Kwa mfano, eneo la Kidabaga linatarajiwa kuwa kitovu kipya cha kiuchumi kutokana na mipango ya kuanzisha kiwanda cha chai. 

Barabara hizi zitakuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha malighafi kutoka mashambani zinafikishwa kwa wakati kiwandani, na pia bidhaa zilizoongezwa thamani kusambazwa kwa urahisi sokoni. 

kufunguka kwa barabara hizi kutachochea ajira kwa vijana, kuongeza pato la wananchi, na kupunguza umasikini katika ngazi ya kaya.

Mbali na kiwanda cha chai, uwepo wa barabara bora unavutia wawekezaji wengine binafsi kuwekeza wilayani humo.

 Mazingira bora ya uwekezaji, ikiwemo miundombinu ya uhakika kama barabara, ni moja ya mambo yanayozingatiwa sana na wawekezaji. 

kwa miaka michache ijayo, Kilolo inaweza kubadilika kutoka wilaya ya kilimo cha kujikimu kwenda kuwa kitovu cha viwanda vidogo na vya kati vinavyoongeza thamani ya mazao ya wakulima.

Kwa upande wa siasa ufanisi huu wa maendeleo umemuweka Mbunge Nyamoga katika nafasi nzuri sana kisiasa. 

Nyamoga anaungwa mkono na wananchi kutokana na jitihada zake za kuhakikisha kuwa ahadi za maendeleo zinatimia. 

Katika mazingira kama haya, ni dhahiri kuwa nafasi ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), inaendelea kuwa imara wilayani humo. 

Kama alivyosema mbunge huyo, ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao si jambo la kujiuliza tena, kwani wananchi wanaona kwa macho yao kazi inayofanywa.

Mbunge Nyamoga pia amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kuunga mkono juhudi za serikali kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, kulinda miundombinu inayojengwa, na kutoa taarifa kwa mamlaka pindi wanapogundua vitendo vya hujuma.

Ikumbukwe kuwa  ushirikiano huu kati ya viongozi na wananchi ndiyo msingi wa mafanikio ya kweli na endelevu.

Hata hivyo mbunge Nyamoga  fursa  amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka msukumo mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati. 

“Rais Samia ni kiongozi wa mfano. Anaonesha upendo na kujali wananchi wake. Kila mkoa, kila wilaya, kila kata sasa inaguswa na miradi ya maendeleo hli ni jambo la kujivunia kama taifa,” alisema.

Alisema kuwa mradi wa barabara ya lami Iringa – Kilolo ni zaidi ya miundombinu ni dira ya matumaini, ni daraja la kiuchumi, na ni alama ya mshikamano kati ya serikali na wananchi. 


Mbunge Nyamoga amekuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha ndoto hizi zinatimia, na kwa hakika, wananchi wa Kilolo hawatamsahau kwa mchango wake katika kuleta mabadiliko ya kweli.

Katika historia ya maendeleo ya Kilolo, jina la Justine Nyamoga litabaki kuwa sehemu muhimu ya simulizi ya mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, yaliyochochewa na uwepo wa barabara bora zinazowaunganisha watu, fursa na maendeleo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI