NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,IRINGA
Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, amesema serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni tisa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami katika eneo la Mkimbizi, ikiwa ni hatua muhimu ya kutatua changamoto ya miundombinu inayowakabili wananchi, hususan wakati wa mvua.
Akizungumza na Matukio Daima TV katika Ofisi za CCM mkoani Iringa, Msambatavangu aliwahakikishia wananchi kuwa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi unaendelea kwa mafanikio, ikiwemo ujenzi wa barabara na miradi mingine ya maendeleo kama soko la kisasa Kihesa.
“Kila mwaka tumekuwa tukifanya ukaguzi na marekebisho ya barabara zisizo na lami, hasa katika maeneo yenye changamoto kubwa kama Mtwivila–Mkimbizi. Baada ya tathmini, tuliamua kutafuta suluhisho la kudumu—ambalo ni ujenzi wa barabara ya lami Zaidi ya bilioni 9 zimetengwa kwa mradi huu, ambao unaweza kuanza wakati wowote,” alisema Msambatavangu.
Aliongeza kuwa serikali haijabaki nyuma kwenye maeneo mengine ya huduma, ikiwemo mchakato wa ujenzi wa soko la kisasa Mkimbizi.
Aliwataka wananchi waendelee kuwa watulivu huku serikali ikiendelea kutekeleza ahadi zake.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo nchini, akisema:
“Kwa kazi anazofanya Rais Samia, anastahili muhula mwingine wa uongozi amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha maendeleo yanawafikia Watanzania kote nchini.”
Kuhusu matumizi ya usafiri wa bodaboda na bajaji na baadhi ya wabunge, Msambatavangu alisema kuwa huo ni mkakati wa kuwasogelea wananchi kwa urahisi:
“Wabunge wengi hutumia bodaboda na bajaji kwa sababu ni njia ya haraka na rahisi kukutana na wananchi. Kuna nyakati tunahitaji kuwa karibu sana na watu wetu, na nyakati nyingine mazingira hutulazimu kutumia magari ya kifahari kutokana na nafasi zetu.”
Kwa upande wake, Richard Samweli, mmoja wa madereva wa bodaboda, alisema ni heshima kubwa kwake kutoa huduma kwa mbunge huyo:
“Najivunia sana kumpakia mbunge wetu. Ni kiongozi mwenye upendo kwa watu hivi karibuni aligharamia matibabu ya dereva mwenzetu aliyepata ajali. Amekuwa msaada mkubwa kwetu kama bodaboda.”
Katika mahojiano hayo, Msambatavangu pia alimpongeza Profesa Mohamed Janabi kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Afya Duniani (WHO) – Kanda ya Afrika, akisema ni heshima kubwa kwa Tanzania na ushahidi wa ubora wa wataalamu wa afya nchini.
MWISHO.
0 Comments