Header Ads Widget

MASHABIKI SIMBA MATUMAINI KIBAO KUBEBA KOMBE SHIRIKISHO

 

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma 

SHABIKI maarufu wa Simba SC,Mbunge wa Nyamagana Stanslus Mabula, ameonesha matumaini makubwa kwa timu yake licha ya kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya RS Berkane katika Uwanja wa Manispaa Berkane nchini Moroco.

Akiongea katika viwanja vya bunge leo Dodoma, amesema kuwa timu ya Simba ina uwezo wa kurekebisha makosa na kufanya vizuri katika mechi ya marudiano, akisisitiza kuwa mpira ni mchezo wa dakika 90 na kila mechi inaweza kubadilika.

"Tumepoteza mechi ya kwanza ya fainali, lakini bado tunaamini kuwa tuna uwezo wa kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano, "

Na kuongeza" Kilichotokea Moroco hakitakuwa kikwazo hapa Tanzania. Simba ni timu kubwa, na tunajivunia kuwa na wachezaji bora ambao wanaweza kurejea kwa nguvu zaidi," alisema Mabula.

Mbunge Mabula ameongeza kuwa mabadiliko ya uwanja yanaweza kuwa na athari kwa utimamu wa wachezaji, lakini Simba kama timu kubwa, imejizatiti kwa mazoezi na maandalizi ambayo yatasaidia kufanya mabadiliko haya kuwa fursa badala ya changamoto.

 Amesisitiza kuwa kwa kutumia uwanja wa nyumbani na ushawishi wa mashabiki, Simba ina nafasi nzuri ya kusonga mbele.

"Tuna imani kwamba kwa msaada wa mashabiki na uwanja wetu wa nyumbani, tutapata matokeo mazuri. Hii ni nafasi ya timu yetu kuonyesha uwezo wake na kutimiza malengo yake," amesema Mabula.

Hata hivyo shirikisho la soka Afrika(CAF) lilionyesha kuwa mchezo wa pili wa fainali ya kombe la shirikisho Afrika utachezwa kwenye uwanja wa New Amaan Complex,Zanzibar ambao ulitumika katika mchezo wa nusu fainali uliozikutanisha Simba na Stellenbosch ya Afrika kusini baada ya uwanja wa benjamini mkapa kuwa katika marekebisho. 

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI