Na,Jusline Marco;Arusha
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro NCAA imetoa mafunzo ya siku mbili kwa wadau wa Utalii kuhusiana na matumizi ya mfumo mpya wa Safari Portal V2 ulioboreshwa kutoka mfumo wa zamani wa Safari Portal.
Akifungua Mafunzo hayo Mei 29, Kaimu Meneja wa Huduma za Utalii na masoko NCAA, Afisa Uhifadhi Mkuu Peter Makutian ameeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wadau wote wa Utalii kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa makusanyo ya mapato yatokanayo na shughuli za Utalii.
Aidha amesema mfumo huo mpya umeboreshwa ili kurahisisha utoaji huduma kwa wadau wote wanaofanya kazi na NCAA,na utaanza kutumia Mei 31 mwaka huu hivyo ni muhimu kwa wadau wote kuwa na kuelewa wa maboresho yaliyofanyika ili kuwasaidia namna ya kuhamisha taarifa zao kwenye mfumo mpya kabla ya tarehe ya kuanza kwa mfumo huo.
Makutian ameongeza kuwa sababu zilizopelekea kuboresha mfumo huo ni kuendana na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano sambamba na kuzingatia mapendekezo ya Wadau wa utalii ambao ndio watumiaji wakuu wa mfumo huo.
Mafunzo hayo yameshirikisha makundi mbalimbali katika mnyororo wa sekta ya utalii ikiwemo Waongoza watalii, wamiliki wa kampuni za utalii, madereva wa utalii, wamiliki wa hoteli na wadau wengine wanaohusika na sekta ya Utalii.
Wadau wa utalii walioshiriki mafunzo hayo wametoa pongezi kwa uongozi wa NCAA kwa maboresho ya mfumo huo ambao umerahisisha taratibu za malipo bila kutumia mda mrefu wanapokuwa na shughuli za utalii na wageni ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
0 Comments