Maafisa wa Syria wakipiga doria karibu na mji mkuu Damascus
Jeshi la anga la Israel limeshambulia karibu na Ikulu ya rais wa Syria mapema Ijumaa baada ya kuonya viongozi wa Syria kutokwenda katika vijiji vinavyokaliwa na jamii za wachache kusini mwa Syria.
Shambulio hilo linakuja baada ya siku kadhaa za mapigano kati ya watu wenye silaha wanaoiunga mkono serikali ya Syria na wapiganaji ambao ni wa madhehebu ya wachache ya Druze karibu na mji mkuu, Damascus. Mapigano hayo yamesababisha makumi ya watu kuuawa au kujeruhiwa.
Shambulio la Ijumaa lilikuwa la pili la Israel dhidi ya Syria wiki hii, na kushambulia eneo karibu na ikulu ya rais inaonekana kutuma onyo kali kwa uongozi mpya wa Syria ambao unaundwa zaidi na vikundi vya Kiislamu vinavyoongozwa na Hayat Tahrir al-Sham.
Siku ya Alhamisi, kiongozi wa kiroho wa Druze wa Syria Sheikh Hikmat Al-Hijri aliikosoa vikali serikali ya Syria kwa kile alichokiita "mashambulizi ya mauaji ya halaiki" dhidi ya jamii hiyo.
Mapema Ijumaa, uongozi wa kidini wa Druze ulisema jumuiya hiyo ni sehemu ya Syria na inakataa kujitenga na nchi hiyo, na kuongeza kuwa serikali inapaswa kuanzisha mamlaka katika jimbo la kusini la Sweida na kudhibiti barabara kuu ya Sweida-Damascus.
Katika kitongoji cha Damascus cha Jaramana, ambako mapigano yalitokea mapema wiki hii, vikosi vya usalama viliwekwa ndani ya eneo hilo pamoja na wapiganaji wa Druze, na baadaye silaha nzito zitakabidhiwa kwa mamlaka. Kama sehemu ya mpango wa amani, vikosi kutoka wizara ya ulinzi vitazunguka Jaramana bila kuingia ndani.
0 Comments