Na Matukio Daima App.
DODOMA.Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, amesema ni jambo la kushangaza kuona vyombo vya ulinzi na usalama havijachukua hatua dhidi ya wanaharakati kutoka nje ya nchi waliokuja Tanzania kufuatilia mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu. 123
Akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 leo bungeni jijini Dodoma,Msambatavangu amesema wanaharakati hao walikuwa na nia ya kuingilia uhuru wa Mahakama, jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.
Ameongeza kuwa vijana wa Kitanzania hawapaswi kuharibiwa kwa ushawishi wa nje, akisisitiza kuwa changamoto zilizopo nchini hazijafikia kiwango cha kuhatarisha amani na usalama wa Taifa.
Aidha Msambatavangu amesema vijana wa Tanzania wamejengwa katika misingi ya amani na haki ndio maana hawawezi kushiriki matendo ya kuharibu amani iliyopo.
"kuna watu wanashangaa utulivu uliopo kwa vijana wa Tanzania bila kujua kuwa vijana hao wamekuzwa kuwa wazalendo"
Msambatavangu amesema Watanzania hawatakubali kuona nchi yao ikivurugwa na majirani au watu kutoka nje wanaotaka kuhatarisha amani.
Msambatavangu amesema kuwa pamoja na changamoto ndogondogo zilizopo, bado hazijafikia kuwa sababu ya kutoheshimiana au kuhatarisha utulivu wa Taifa.
"Tanzania bado ni kisiwa cha amani,hao wanaotutukana majukwaani na mitandaoni, wakipata matatizo wao ndio wa kwanza kutegemea wakimbilie Tanzania," amesema.
Amesisitiza kuwa vijana wa Kitanzania hawatajiingiza katika mambo ya 'kipumbavu', yanayoweza kuvuruga nchi, huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kuiheshimu na kuilinda amani iliyopo.
MWISHO.
0 Comments