Tanzania na PUMA kuimarisha ushirikiano
PUMA kuendelea kuwekeza zaidi Tanzania
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nishati ya PUMA Energies, Duniani Bw. Mark Russell.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Mei 27, 2025 jijini Dodoma, Dkt. Biteko ameipongeza Kampuni ya PUMA Energies kwa kuwekeza nchini na kutoa huduma ya viwango vya juu katika bidhaa zake pamoja na kuzingatia wazawa katika nafasi za juu za utendaji za Kampuni hiyo nchini.
Vilevile, ametoa rai kwa PUMA Energies kuendelea kuwekeza zaidi nchini na kusema kuwa Kampuni hiyo inaweza kujenga vituo zaidi vya kuweka gesi kwenye magari ili kusaidia upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Kuhusu nishati safi ya kupikia, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Kampuni ya PUMA kuwekeza katika eneo hilo na kusema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano wake kwa Kampuni hiyo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nishati ya PUMA Energies, Bw. Mark Russell amesema kuwa Kampuni yake imewekeza zaidi ya dola za kimarekani milioni 24 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitatu vya kujaza gesi kwenye magari katika mikoa ya Dar es salaam na kimoja Dodoma.
MWISHO.
0 Comments