Na Matukio Daima Media, Kondoa
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kuteketeza Ekari 157 za mashanba ya bangi katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Naibu Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano ya Serikali wa MAMLAKA hiyo, Daniel Kasokola alisema operesheni maalum kwa kushirikiana na Mamlaka, Kamati ya Ulinzi ya wilaya pamoja na wananchi wa Kata ya Haubi imefanikiwa kutokomeza kilimo haramu cha bangi katika Hifadhi ya Milima ya Haubi, wilayani humo.
Kasokola amesema operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia Mei 14 hadi 19, mwaka huu imefanikisha uteketezaji wa ekari 157 za mashamba ya bangi yaliyokuwa katika vijiji vya Ntomoko, Kinyasi na Haubi.
Pia, wanawashikilia watuhumiwa saba kwa mahojiano, wamekamata pikipiki mbili katika maeneo ya operesheni hiyo.
“Operesheni hii ni ya pili kufanyika mwaka huu katika Wilaya ya Kondoa. Januari mwaka huu tulibaini na kuteketeza zaidi ya ekari 500 za bangi. Hii ni awamu ya pili katika wilaya hii, kupungua kwa mashamba haya hadi ekari 157 ni ushahidi kuwa wananchi wameanza kuelewa na kushiriki kikamilifu katika jitihada hizi, tunaomba wananchi waendelee na ushirikiano huu.” amesema Kasokola.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatuma Nyangassa, amesisitiza kuwa serikali ya wilaya itaendelea kushirikiana kwa karibu na DCEA katika kuhakikisha kilimo cha bangi kinatokomezwa kabisa na kusisitiza kuwa elimu kwa wananchi itaendelea kutolewa ili waachane na kilimo hicho haramu na badala yake wajikite katika uzalishaji wa mazao halali ya chakula na biashara kama vile tumbaku, ufuta na maharage.
“Tunawaomba wananchi waachane na kilimo haramu cha bangi. Serikali ipo tayari kuwaongoza katika kuelekea kilimo halali na chenye tija. Ushirikiano baina ya serikali na wananchi ndiyo silaha kubwa ya kuikomboa jamii yetu.” amesisitiza Nyangasa.
kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mafai, Shaibu Hamis Kalinga, ameweka bayana kuwa kijijini hapo kumekuwa na
historia ya kilimo cha bangi kwa muda ndefu, lakini kwa sasa viongozi wa kijiji wamejipanga kuongoza mapambano dhidi ya zao hilo haramu.
“Zamani bangi ilikuwa kama sehemu ya maisha kwa baadhi ya wakulima hapa kijijini, lakini sasa tunaelewa madhara yake. Tumejipanga kutoa elimu na kuhamasisha kilimo halali tu.” alisema Kalinga
Naye Rajabu Hamis, mkazi wa kijiji cha Mafai, amepongeza juhudi za serikali kwa kutoa elimu kwa Wananchi jambo ambalo limebadili fikra za wananchi kuhusu bangi.
“Tulilima bangi kwa sababu ya kukosa njia mbadala, lakini baada ya kupewa elimu na kuona jitihada za serikali, tumeamua kuachana na bangi na kushirikiana na mamlaka kuitokomeza kabisa" alifafanua Rajab
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambna na Dawa za Kulevya itaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayejihusisha na kilimo, biashara au usambazaji wa bangi na dawa nyingine za kulevya.
0 Comments