Na Fatma Ally, Matukio Daima Media
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kufanya mkutano mkuu maalum wa CCM Taifa Mei 29 na 30 jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es Salaam mapema leo hii, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo (CCM) Taifa, CPA. Amos Makalla,amesema mkutano huo utakua na ajenda 3 ikiwemo kupokea taarifa ya ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/ 2025 Tanzania Bara na Visiwani.
Amesema kuwa, ajenda nyengine ni kupokea na kuzindua rasmi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030,itakayotumika katika kipindi cha kampeni za chama pamoja na kufanya karekebisho madogo ya katiba ya CCM.
Amesema kuwa, CCM imejipanga vizuri katika kusimamia ilani ya uchaguzi hivyo, haina shaka kushinda katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika October mwaka huu.
Aidha, amesema wananchi watarajie ilani inayokidhi mahitaji ya wananchi, hususani maendeleo maendeleo ya Jamii kwani mara zote wamekua wakitoa ilani bora ambayo inamjali mwananchi.
Pia amesema kuwa, CCM inaamini katika kushinda kwenye uchaguzi mkuu kutokana na kuwa na ilani inayokidhi mahitaji ya wananchi katika vipindi vyote.
Hata hivyo, amewataka wadau mbalimbali kujitokeza katika mkutano huo wakiwemo wajumbe wa halmashauri kuu, makada wa Chama ili kuskiliza mambo mazuri yatakayozingumzwa katika mkutano huo.
Aidha ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha nyingi za maendeleo, katika sekta ya afya, elimu,miundombinu ya barabara,maendeleo ya jamii na nyingine.
"Katika awamu hii ya sita Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo kila Kijiji, kitongoji, kata, Jimbo na Wilaya imefika kutatua kero za wananchi"amesema CPA Makalla.
0 Comments