Na Matukio Daima App.
DODOMA.WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa amesema wamejipanga kwa vitendea kazi na utimamu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu unafanyika kwa amani huku akionya atakaefanya fujo atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo ameitoa leo Mei 21 bungeni Jijini wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Malinyi, Antipas Mgungusi (CCM) ambaye alitaka kujua lini Serikali italipatia magari Jeshi la Polisi Malinyi ili liweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Waziri Bashungwa amesema kuelekea uchaguzi Mkuu wamejipanga kuhakikisha unafanyika kwa amani huku akionya kwa wale wenye chokochoko katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu dawa yao imepatikana.
"Na nitumie nafasi hii kuwaambia watanzania tumejipanga ipasavyo katika uchaguzi wa mwaka huu na tutahakikisha unafanyika kwa amani na usalama. Na tumejipanga kwa vitendea kazi pamoja na utimamu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha kila atakayepanga kufanya fujo anashughulikiwa kwa mujibu wa sheria," amesema Waziri Bashungwa
Aidha, Waziri Bashungwa pia amesema Serikali inapeleka magari ya wapelelezi wa Wilaya na ikifika Agosti mwaka huu watayasambaza nchi nzima kila wilaya ili kuimarisha ulinzi na usalama.
MWISHO.
0 Comments