Na Ashrack Miraji Matukio Daima App
Benki ya NMB tawi la Same imeonesha tena moyo wa uwajibikaji kwa jamii kwa kukabidhi msaada wa vifaa vya kuandikia kwa wanafunzi wa kidato cha sita ambao wanaanza mithihani ya Taifa wiki hijayo Tukio hilo limefanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Same ambapo viongozi wa benki hiyo walikabidhi rasmi vifaa hivyo kwa uongozi wa shule pamoja na baadhi ya wanafunzi.
Msaada huo ulihusisha vifaa mbalimbali ikiwemo kalamu, rula vifutio na penseli za kuchora. Lengo la msaada huo ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanajiandaa vizuri kwa mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita, ambayo ni hatua muhimu kuelekea elimu ya juu. Benki hiyo imesisitiza kuwa wanaamini elimu ni ufunguo wa maendeleo ya jamii.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja wa NMB tawi la Same Saad Masawila alisema kuwa benki yao imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia sekta ya elimu kwa miaka mingi, na kwamba msaada huo ni sehemu ya mpango wao wa uwajibikaji kwa jamii (CSR). “Tunaamini wanafunzi wetu wakipewa mazingira bora ya kujifunzia na kufanya mitihani, wataweza kufanya vizuri zaidi na hatimaye kuisaidia jamii yao,” alisema Masawila
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Same, Mwl. Mbuki A. Mbuki ameipongeza Benki ya NMB kwa msaada huo akisema kuwa umetolewa kwa wakati muafaka. Aliongeza kuwa shule nyingi za serikali hukumbana na changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya kutosha kwa wanafunzi, hasa kipindi cha mitihani, na kwamba msaada huo umepunguza kwa kiasi kikubwa mzigo huo.
Wanafunzi waliopokea msaada huo walionesha furaha yao huku wakitoa shukrani kwa benki ya NMB. Mmoja wa wanafunzi hao, Majaba Mayuma alisema kuwa msaada huo umewatia moyo na kuwapa ari ya kufanya vizuri kwenye mitihani yao. “Tunajisikia kuthaminiwa na kujaliwa, tunawaahidi kufanya vizuri ili kuonyesha kuwa msaada huu haujaenda bure,” alisema Amina.
Katika hitimisho la hafla hiyo, viongozi wa shule na jamii waliitaka benki hiyo kuendelea na moyo huo wa kusaidia, si tu kwa wanafunzi wa kidato cha sita, bali pia kwa ngazi nyingine za elimu. Waliitaka pia jamii nzima kuiga mfano huo na kushirikiana kuinua sekta ya elimu nchini.
Mbali na msaada wa vifaa vya mitihani, benki ya NMB imeahidi kuangalia uwezekano wa kuanzisha programu maalum za kifedha kwa wanafunzi, ili kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya fedha na kujitegemea. Mawasila alieleza kuwa elimu ya fedha ni muhimu kwa vijana hasa wanapokaribia kumaliza elimu ya sekondari na kuingia katika maisha ya kujitegemea.
Aidha, Benki ya NMB imeweka wazi kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wengine wa elimu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kufanikisha ndoto zao. Hii ni sehemu ya mpango wao wa muda mrefu wa kusaidia maendeleo ya kijamii kupitia uwekezaji katika sekta muhimu kama elimu, afya na ujasiriamali.
Katika ujumbe wa pamoja uliotolewa na walimu, wazazi na wanafunzi, waliishukuru NMB kwa kuwa mfano wa taasisi zinazojali maendeleo ya elimu. Walisisitiza kuwa msaada huo hautasaidia tu kwenye mitihani ya sasa, bali umeacha alama ya matumaini kwa vizazi vijavyo.
0 Comments