Na Moses Ng’wat, Songwe.
Vyombo vya dola mkoani Songwe vimeagizwa kufuatilia kwa karibu malalamiko dhidi ya watendaji na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) wanaojihusisha na udanganyifu katika biashara ya zao la ufuta, ikiwemo kuchanganya mchanga ili kujipatia fedha kwa njia isiyo halali.
Agizo hilo limetolewa Aprili 24, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya ufuta kilicholenga kujadili mifumo ya masoko na kuzindua rasmi msimu wa ununuzi wa zao hilo kwa mwaka 2024/25.
“Kumekuwa na michezo na rafu nyingi kwenye biashara hii ya ufuta. Nitoe wito kwa wote wanaohusika na mnyororo mzima wa thamani ya zao hili kuwa waadilifu. Vyombo vya dola viwe macho na kuchukua hatua dhidi ya kila aina ya udanganyifu,” alisema Chongolo.
Alifafanua kuwa baadhi ya viongozi na watendaji wa AMCOS wamekuwa wakiongeza mchanga kwenye ufuta uliokusanywa kutoka kwa wakulima kwa nia ya kujiongezea faida, hali inayoharibu sifa na soko la zao hilo katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, alionya kuhusu tabia ya baadhi ya viongozi wa vyama hivyo na watunza maghala wasio waaminifu wanaosajili mizigo hewa kwa kuingiza majina na akaunti za wakulima wasio na ufuta kwenye mfumo wa masoko, jambo linalosababisha malipo kufanyika kwa mizigo isiyokuwepo.
Amesisitiza kuwa wakulima wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda ubora wa mazao yao kwa kufuata kanuni bora za kilimo na kuhakikisha usafi wa mazao ili kupata soko la uhakika.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Chongolo, katika msimu wa mwaka 2023/24, Mkoa wa Songwe ulizalisha jumla ya tani 12,423.581 za ufuta na kupata mapato ya Shilingi 1,400,409,707.49. Kati ya hizo, tani 8,404.331 zilikuwa kutoka Wilaya ya Songwe ambapo wakulima walilipwa Shilingi 961,161,579.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Kamwesige Mtembei, alisema kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani na matumizi ya minada ya kidijitali katika mwaka 2024 umeonesha mafanikio makubwa, ukiwanufaisha wakulima kwa kuongeza uwazi na ushindani wa bei.
0 Comments