Header Ads Widget

RAIS SAMIA AIKARIBISHA MAN UTD KUWEKEZA TANZANIA

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa Klabu ya Manchester United ya Uingereza, Sir Jim Ratcliffe, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 11 Aprili, 2025, ambapo amemkaribisha rasmi kuwekeza katika sekta za michezo na utalii nchini.

Mazungumzo hayo yalijikita katika fursa za ushirikiano baina ya Tanzania na Manchester United, klabu yenye mashabiki mamilioni duniani, wakiwemo wengi kutoka barani Afrika.

Sir Jim ameonesha nia ya kuitumia klabu hiyo kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kimataifa, hususan kupitia kampeni za utalii.

Aidha, Rais Samia alipokea zawadi ya jezi ya Manchester United iliyosainiwa na wachezaji wa timu hiyo, kama ishara ya heshima na urafiki kutoka kwa mmiliki huyo wa klabu.

Rais Samia alitumia fursa hiyo kumualika Sir Jim kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya mafunzo ya michezo (Sports Academies) nchini, ili kuwawezesha vijana wa Kitanzania kukuza vipaji vyao na kushiriki kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Manchester United tayari imekuwa ikifanya kazi na mashirika na mataifa mbalimbali barani Afrika, ikiwemo miradi ya kijamii kupitia Manchester United Foundation, lakini hii ni mara ya kwanza kwa mmiliki wa klabu hiyo kuonesha nia ya uwekezaji wa moja kwa moja katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ziara ya Sir Jim Ratcliffe nchini Tanzania ni hatua muhimu inayoweza kufungua milango kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta ya michezo na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia diplomasia ya michezo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI