Header Ads Widget

NAIBU WAZIRI MKUU DKT DOTTO BITEKO ATOA RAI YA KUDUMISHA TUNU YA MUUNGANO - ARUSHA


Na,Jusline Marco;Arusha

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amewasihi Watanzania kuenzi na kudumisha tunu ya Muungano ulioasisiwa na waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, akisisitiza kuwa amani na mshikamano wa Taifa ni nguzo muhimu ya maendeleo.

Akizungumza Leo  katika mkutano wa hadhara wilayani Arumeru, mkoani Arusha, Dk. Biteko alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha maendeleo yanamfikia kila Mtanzania, huku akibainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 100 zimetolewa kwa halmashauri za Arusha na Meru kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Halmashauri ya Arusha imepokea shilingi bilioni 49 na Meru zaidi ya bilioni 52. Haya ni maendeleo yanayoonekana kwa macho. Tunapaswa kuilinda amani yetu kwa gharama yoyote, kwani Tanzania ni nchi pekee ambako watu wa dini zote na wasiokuwa na dini wanaishi kwa mshikamano,” alisema Dk. Biteko.

“Wapo wanaosema tupigane kidogo. Hii si hoja. Amani inalindwa kwa gharama kubwa. Tusiichezee,” alisisitiza.

Kuhusu miundombinu, Naibu Waziri Mkuu alieleza kuwa serikali inatarajia kupanua barabara ya Arusha–Tengeru kuwa ya njia nne ili kupunguza msongamano na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. 

Alisema serikali inaendelea kuwekeza kwenye sekta muhimu kama nishati, elimu na afya, ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

“Tanzania sasa inatimka vumbi kwa miradi ya maendeleo. Serikali inasikiliza na kutatua kero za wananchi. Hii ni dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo.”

Katika ziara hiyo, Dk. Biteko aliweka jiwe la msingi kwenye jengo la utawala la Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 5.664. Mradi huo unatekelezwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ukitarajiwa kukamilika Mei 17, 2025.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha TCDI, Dk. Bakari George, amesema hadi sasa ujenzi huo umeshagharimu shilingi bilioni 2.7. Jengo hilo litakuwa na ghorofa tatu, sakafu nne, ofisi 44 na kumbi tano zitakazochukua watu 545 kwa wakati mmoja.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI