Mwanamke mmoja nchini Australia amejifungua mtoto wa mtu asiyemfahamu bila kujua, baada ya kliniki yake ya uzazi kuingiza kwa bahati mbaya viinitete vya mwanamke mwingine ndani ya chake.
Mchanganyiko huo katika kliniki ya kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi ya Monash IVF huko Brisbane, Queensland umesemekana kuwa makosa ya kibinadamu, vyombo vya habari vya Australia vinaripoti.
"Kwa niaba ya Monash IVF, nataka kusema ninasikitika sana kwa kile kilichotokea," Mkurugenzi Mtendaji Mkuu Michael Knaap alisema, akiongeza kwamba kila mtu katika kliniki ya uzazi "alihuzunishwa" na kosa hilo.
Mwaka jana, kliniki hiyo hiyo ililipa A$56m (£26.8m) kwa mamia ya wagonjwa ambao viinitete vyao viliharibiwa licha ya kuwa na uwezo wa kutungisha mimba.
Kulingana na msemaji wa Monash IVF, wafanyikazi walifahamu tatizo hilo mnamo mwezi Februari wakati wazazi waliozaa walipoagizwa kuhamisha viinitete vyao vilivyobaki vilivyogandishwa hadi kliniki nyingine.
"Badala ya kupata idadi inayotarajiwa ya viinitete, kiinitete cha ziada kilibaki kwenye hifadhi," msemaji huyo alinukuliwa akisema na ABC.
Monash amethibitisha kwamba kiinitete kutoka kwa mgonjwa mwingine kiliyeyushwa kimakosa na kuhamishiwa kwa mtu tofauti, na kusababisha kuzaliwa kwa mtoto.
Kliniki imeanzisha uchunguzi na tukio hilo limeripotiwa kwa vyombo vya udhibiti.
0 Comments