Mzaliwa wa Dublin, Farrell alitumia zaidi ya miaka 30 kufanya kazi nchini Marekan
Baada ya ulimwengu kutaarifiwa kuwa Papa Francis amefariki asubuhi ya Jumatatu, Kadinali Mmarekani , ambaye hajatambuliwa na wengi duniani , alipasua mbarika kuhusu kifo cha Papa.
Baada ya kutangaza kuwa Papa amerejea ''nyumbani kwa baba yake'' ikiwa na maana ameaga dunia Kadinali ambaye ni Ireland Mmarekani Kevin Farrel alichukua jukumu kubwa: Camerlengo'' wadhifa ambao mtu anahudumu kama kiongozi wa Vatican baada ya kifo au kustaafu kwa Papa.
Papa Francis alimteua kwa wadhifa huo mwaka 2019. Kadinali huyu atabaki katika wadhifa huo kipindi hiki cha majonzi hadi uchaguzi uandaliwe wa mkuu wa kanisa la katoliki.
Pia atasimamia na kuongoza desturi zote ambazo hufanywa katika maombolezi ya Papa Francis.
Kadinali Kevin Farrell alizaliwa mwaka 1947 mjini Dublin, Ireland.
Alipata elimu yake ya juu katika Chuo Kikuu cha Salamanca nchini Hispania na baadaye katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, Roma, kwa mujibu wa taarifa kutoka Vatican.
Katika maisha yake ya huduma ya kidini, Farrell alihudumu katika maeneo mbalimbali duniani.
Aliwahi kuwa mchungaji wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Monterrey nchini Mexico na pia kuhudumu katika parokia ya Bethesda, Maryland, Marekani.
Kwa zaidi ya miaka 30, Farrel mwenye umri wa miaka 77 aliendelea kuhudumu katika majimbo na parokia nchini Marekani, akijenga sifa ya uongozi thabiti na wa kujitolea.
Mwaka 2007, aliteuliwa kuwa Askofu wa Dallas, nafasi aliyoishikilia hadi mwaka 2016, ambapo Papa Francis alimteua kuwa mkuu wa idara mpya ya Vatican inayosimamia huduma ya kichungaji kwa familia.
Uteuzi huo pia ulimuinua hadi ngazi ya Kadinali.
Miaka baada ya kuteuliwa kama Camerlengo, mwaka 2023, Papa Francis aliongeza majukumu yake kwa kumteua kuwa Rais wa Mahakama ya Juu ya Mji wa Vatican, pamoja na kuwa Rais wa Tume ya Masuala ya Siri (Commission for Confidential Matters).
Jukumu la Camerlengo
Kama Camerlengo, Kadinali Farrell atakuwa na jukumu la kuandaa mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya — maarufu kama conclave.
Ni katika mchakato huu ambapo makadinali hukutana kwa siri na kumpigia kura Papa ajaye.
Ingawa si jambo la kawaida, camerlengo anaweza kuchaguliwa kuwa Papa, na historia imeshuhudia hali hiyo mara mbili: kwa Gioacchino Pecci (aliyekuwa Papa Leo XIII) mwaka 1878 na Eugenio Pacelli (aliyekuwa Papa Pius XII) mwaka 1939.
Kama sehemu ya majukumu yake, Kadinali Farrell pia atasimamia kuthibitisha rasmi kifo cha Papa Francis, kuweka mwili wake kwenye jeneza, na kuongoza msafara wa heshima ya mwisho kutoka kapela ya Domus Santa Marta hadi Basilika ya Mtakatifu Petro.
Kwa mujibu wa Vatican, ibada hiyo ya mwisho inaweza kufanyika mapema siku ya Jumatano asubuhi.
0 Comments