Na Fadhili Abdallah, Kigoma
Shule za Msingi, Sekondari na nyumba za ibada katika jimbo la Buhigwe wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma zinatajia kunufaika na huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kufuatia mpango wa mbunge wa jimbo hilo kujenga visima kwa taasisi za elimu na nyumba za ibada.
Mbunge wa jimbo la Buhigwe, Felix Kavejuru alisema hayo akihutubia mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Rusaba wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma ambapo amesema kuwa visima Zaidi ya 90 vinatarajia kujengwa katika mpango huo vikihusisha pia kupeleka visima hivyo kwenye zahanati na vituo vya afya.
Kavejuru alisema kuwa uchimbaji huo wa visima katika nyumba za ibada na taasisi za elimu ni sehemu ya mpango wa kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji katika jimbo hilo na kwamba utekelezaji wa mpango huo utaanza muda si mrefu baada ya kukubaliana na wafadhili kutoka nchini Korea.
Mbunge huyo wa jimbo la Buhigwe alisema kuwa mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa kusogeza karibu huduma ya maji safi na salama karibu na wanchi wakati mradi mkubwa wa vijiji vinane wenye thamani ya shilingi Bilioni 9.7 ukiendelea na unatarajia kukamilika muda si mrefu.
Sambamba na hilo Mbunge huyo alisema kuwa tayari Rais Samia kupitia wizara ya maji na Wakala wa maji mijini na vijijini (RUWASA) imetoa kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya uchimbaji visima vitano kwenye jimbo hilo na yayari ameshatoa maelekezo ya wapi visima hivyo vichimnbwe na kazi imeanza.
baadhi ya wananchi wa jimbo hilo Shadrack Hamenya mkazi wa kijiji cha Rusaba walisema kuwa pamoja na taarifa hizo bado tatizo la upatikanaji kwa sasa ni kubwa hivyo wanaiomba serikali ikamilishe miradi hiyo kwa vitendo badala ya kuwa mambo ya siasa kwani huduma ya maji haitaki siasa ni maisha ya wananchi.
mwisho.
0 Comments