Na Matukio Media
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Festo Kiswaga, ametoa onyo kali kwa Wenyeviti wa Vijiji katika Wilaya hiyo akiwataka kuacha mara moja tabia ya kufanya vikao vya kijiji au maamuzi yoyote ya kiutawala bila kushirikisha au kutoa taarifa kwa Watendaji wa Vijiji.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika siku ya jana uliowakutanisha Wenyeviti wa Vijiji na Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha utendaji wa viongozi hao katika kuwahudumia wananchi kwa weledi na kuzingatia sheria.
Katika maelekezo yake Kiswaga alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakifanya maamuzi nyeti ya kijiji bila kushirikisha Watendaji, hali ambayo ni kinyume na taratibu za utawala bora.
Alisisitiza kuwa mtendaji ni sehemu ya serikali anayeiwakilisha mamlaka za juu katika ngazi ya kijiji, hivyo lazima ahusishwe katika kila kikao rasmi au maamuzi yoyote yanayogusa wananchi.
“Kuanzia sasa ni marufuku kabisa kufanyika kwa kikao chochote cha kijiji bila taarifa kwa Mtendaji Hii siyo siasa, huu ni uongozi wa kisheria na lazima tuheshimu muundo wa utawala Mtendaji ni kiungo muhimu kati ya serikali na wananchi,” alionya Mhe. Kiswaga.
Kiswaga pia alikemea vikali vitendo vya uuzaji wa ardhi kiholela vinavyofanywa na baadhi ya wenyeviti bila kushirikisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri.
Alisema hatua hiyo ni chanzo kikuu cha migogoro ya ardhi katika maeneo mengi ya Monduli.
“Sitavumilia kuona ardhi ya wananchi ikiuzwa bila kufuata utaratibu. Ardhi si mali ya mtu binafsi, lazima kila uamuzi kuhusu ardhi upitie ngazi husika kwa mujibu wa sheria,” alisema kwa msisitizo.
Aidha Kiswaga alisisitiza umuhimu wa Viongozi hao kushirikiana katika utendaji, sambamba na kutambua kuwa wananchi ndio waajiriwa wao, akivitaka pia vyombo vya habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa kuweka usawa kwenye taarifa zao kwa kuzungumza na pande zote zitakazokuwa zinahusika na taarifa wanazoziandika kutoka kwa wananchi.
"Kila mmoja lazima uoneshe uwezo wako wa kiuongozi kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizopo, kuna watu wanashinda Uenyekiti wa Kijiji anaona kama kile Kijiji ni cha kwake, cha familia yake na anaweza kufanya chochote anachotaka.
Kazi haziendi hivyo, kama uliingia ukakuta mipango ya mwenzako imefanyika, usiiguse isipokuwa tu kama ilikuwa ina tatizo, mfuate Mtendaji muulize na baadae iboreshe tu kwa kushirikisha wenzako."
Katika upande mwingine baada ya mkutano huo, baadhi ya viongozi waliokutana na Mkuu wa Wilaya walionesha kuridhishwa na maelekezo yaliyotolewa, wakisema kuwa yamewapa mwanga na uelewa wa kina juu ya wajibu wao kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha loseiro Yamati Laizer alisema “Tumekuwa tukifanya baadhi ya maamuzi kwa mazoea bila kujua kuwa tunavunja taratibu.
Maelekezo haya yametufumbua macho na tunaahidi kushirikiana na Watendaji wetu kwa karibu zaidi.”
Fatuma Ramadhani, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mti Moja, alisema "Mkutano huu umekuwa wa muhimu sana kwetu sisi watendaji.
Tumepata uelewa mzuri kuhusu nafasi yetu katika uongozi na ushirikiano wetu na viongozi wa vijiji. Tutaendelea kutoa msaada wa kisheria na usimamizi bora wa shughuli za kijiji ili kuhakikisha kila hatua inayochukuliwa inazingatia sheria na miongozo ya Serikali."
0 Comments