Habari na Matukio Daima App.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe CPA. Cecilia Kavishe, amezindua kampeni ya mradi wa kuwarudisha watoto shule ambao hawapo shuleni kutokana na sababu mbalimbali katika Wilaya ya Songwe.
Kampeni hiyo ambayo imezinduliwa jumanne Aprili 8, 2025 inafanywa na Serikali katika Wilaya ya Songwe kwa kushirikiana na shirika linalohudumia watoto duniani UNICEF.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo CPA. Kavishe amewataka watendaji wa kata, vijiji na wenyeviti wa vitongoji kuhakikisha watoto wote kuanzia miaka saba hadi 14 ambao hawapo katika mfumo wa elimu rasmi wanarudi shuleni.
Mkurugenzi huyo mtendaji wa Halmashauri ya Songwe, amesema baadhi ya watoto wanaacha shule kutokana na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji na uchimbaji madini hivyo amewasisitiza viongozi hao kuangalia maeneo hayo ambayo yamekuwa yakichangia watoto kuacha masomo.
Katika kikao hicho, CPA. Kavishe sanjari na kuhimiza ufuatiliaji wa watoto hao, pia amewaagiza viongozi wa kata, vijiji na vitongoji kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
“Naamini kila eneo kuna miradi inatekelezwa. Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ameleta fedha nyingi katika Halmashauri yetu (Songwe). Lazima viongozi mfuatilie, mjue nini kinafanyika katika maeneo yenu” amesema Cesilia Kavishe mkurugenzi Halmashauri ya Songwe.
Malengo ya kampeni hiyo ni kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu, kuwajengea watoto fikra na kuwajengea misingi bora katika nyanja zote za kimaisha.
Kavishe amebainisha kuwa kampeni hiyo yenye kauli mbiu ‘Elimisha Mtoto’ ambayo ilianza katika kata tano, inatarajia kuwarejesha zaidi ya watoto 300 ambao wapo nje ya mfumo rasmi wa elimu kuhakikisha wanarudi kupata elimu kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
0 Comments