Na WAF - Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imeishauri Serikali kupitia Wizara ya Afya iendelee kukutana na wadau wa Sekta Binafsi ikiwemo wamiliki wa hospitali ili kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kutengeneza utaratibu wa Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ya mwaka 2025 katika kuelekea utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi Mhe. Cecil Mwambe ametoa pendekezo hilo Machi 8, 2025 baada ya Serikali kutoa ufafanuzi kuhusu hoja za Kamati hiyo katika muswada wa mabadiliko ya sheria ya mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wa Mwaka 2025 zilizowasilishwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama katika kumbi za Bunge Jijini Dodoma.
"Sisi kama Kamati tunaishauri Serikali kupitia Wizara ya Afya, iendelee kukutana na wadau wake wakiwemo wamiliki wa hospitali na taasisi binafsi ili muweze kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ya Mwaka 2025 inayopendekezwa ili iweze kuwa na manufaa zaidi kwa wananchi," amesema Mhe. Mwambe
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kwa kuwa wadau hao sio washindani wa Serikali bali ni washirika kwa kuwa na lengo moja la kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Nimeendelea kusema na kusisitiza kuwa sisi (Serikali) sio washindani wa sekta binafsi bali sisi ni washirika kwa kuwa tuna lengo moja kubwa la kuwahudumia wananchi, lakini pia tumepokea maelekezo ya kamati na tutaenda kuyafanyia kazi," amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji mkubwa wa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya elfu 10,044 nchi nzima ambavyo vimewezesha wananchi kupata huduma za afya ndani ya kilometa tano (5).
"Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa ambapo mwananchi akitembea ndani ya kilometa tano (5) anapata huduma za afya na sasa tunaendelea kupitia tena miongozo ili sekta binafsi iweze kusaidia kutoa huduma za afya angalau tupunguze zaidi umbali wa kupata huduma hizi," amesema Waziri Mhagama
Nae, Mwanasheria wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Matamusi Fungo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu hoja za kamati amesema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unayo mikakati mbalimbali ya kuhakikisha unakuwa na uhai na uendelevu ikiwa ni pamoja na kufanya tathimini kila baada ya miaka mitatu (3) kwa mujibu wa sheria na kuzingatia mapendekezo ya tathmini hiyo.
"Lakini pia kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya wanachama, wategemezi, waajiri, watumishi wa mfuko pamoja na vituo. Mfuko kuendelea kudhibiti matumizi ya gharama za uendeshaji kwa kuzingatia kifungu cha 33 (1) (b) cha Sheria ya Mfuko," amesema Bw. Fungo
0 Comments