Header Ads Widget

MPANGO WA KUGAWA BURE VYANDARUA MIL.1.5 WAZINDULIWA KIGOMA.



 


 


Na Fadhili Abdallah


 


ZAIDI ya vyandarua milioni 1.5 vinatarajia kugawiwa bila malipo kwa wananchi wa mkoa Kigoma ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini.


 


Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Hassan Rugwa alisema hayo  wakati akizindua zoezi la mkoa la uhamasishaji na utoaji elimu kwa jamii kabla kuanza kwa zoezi la ugawaji ambapo alisema kuwa zoezi hilo ni muhimu kwa mkoa Kigoma kutokana na changamoto ya kijiografia ambapo mkoa huo upo mpakani ukipakana na nchi za ukanda wa maziwa makuu ambazo zinasumbuliwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa huo .


 


Rugwa alisema kuwa pamoja na nchi hizo kusumbuliwa na maralia bado  serikali ya Tanzania haijui afua ambazo nchi hizo zinachukua na ndiyo maana serikali imeona ichukue hatua katika kuwakinga na kuwalinda watu wake huku akibainisha kuwa mkoa Kigoma kwa sasa una asilimia 13 ya maambuki ya ugonjwa huo kwa watu wake.


 


Akitoa maelezo katika uzinduzi huo  afisa kutoka idara ya udhibiti wa malaria ya wizara ya afya, Wilfred Mwafongo alisema kuwa zoezi hilo limezinduliwa rasmi mkoani Kigoma kwa kuanza na elimu na umasishaji kwa makundi mbalimbali, litafuata zoezi la usajili wa kaya na baadaye ugawaji wa vyandarua bila malipo utafanyika na kwamba mkoa Kigoma ni moja ya mikoa tisa itakayotekeleza zoezi kutokana na takwimu kuonyesha mikoa hiyo ina idadi kubwa ya wagonjwa wa maralia nchini.


 


Akizungumza katika uzinduzi huo Mratibu wa malaria mkoa Kigoma, Cresensia John alisema kuwa pamoja na mpango wa ugawaji wa vyandarua kwa kaya ambapo kila watu wawili katika kaya watapewa chandarua kimoja pia wanatarajia kunyunyizia dawa ya kuua vimelea vya malaria na tayari lita 25,000 zimeagizwa kwa ajili ya kazi hiyo.


 


Mwisho.


Afisa kutoka Idara ya Udhibiti wa Malaria kutoka Wizara ya Afya, Wilfred Mwafongo akizungumza katika uzinduzi wa zoezi la uhamasishaji na ugawaji vyandarua bure kwa wananchi wa mkoa Kigoma.


Cresensia John Mratibu wa Malaria mkoa Kigoma.


Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Hassan Rugwa akiongea katika zoezi la uzinduzi wa uhamasishaji na ugawaji vyandarua bila malipo kwa wananchi wa mkoa Kigoma.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI