Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Siku chache baada ya uongozi wa timu ya Mashujaa kutangaza benchi jipya la ufundi kufuatia kumtimua kocha wake Mohamed Barres wachezaji wa timu hiyo wamesema kuwa bado wanaamini malengo yao ya kuifanya timu hiyo kushika nafasi ya nne za juu katika msimamo wa ligi ya NBC nchini uko pale pale.
Wakizungumza na waandishi wa habari wachezaji wa timu hiyo walisema kuwa wanaamini kuwa kocha mpya aliyetangazwa na uongozi wa timu hiyo Salum Mayanga anayo nafasi yake katika kuwavusha katika michezo saba iliyobaki ya kumaliza ligi kuu ya NBC nchini.
Mmoja wa wachezaji hao Luben Lyanga alisema kuwa ujio wa kocha mpya Salum Mayanga kwao ni jambo la kawaida kwa uongozi unapoona ipo sababu ya kufanya hivyo hasa katika kupata matokeo hivyo wanampokea kocha kwa mikono miwili na watafanya naye kazi kulingana na mpango kazi wake na falsafa aliyokuja nayo.
Naye Mshambuliaji Mohamed Mussa alisema kuwa mabadiliko ya uongozi katika benchi la ufundi ni kawaida na bahati mbaya wamefanya vibaya hadi sasa kwenye msimamo wa ligi ya NBC lakini baada ya mapumziko ya mechi za Timu za Taifa wanarudi na nguvu mpya na ari mpya na kila watakayekutana naye sasa ni fainali.
Kwa upande wake Mshambuliaji Chrispin Ngushi alisema kuwa mechi ya kwanza ambayo wanataka kuirudisha timu kwenye nafasi yake ni mechi dhidi ya Pamba Jiji kwenye mashindano ya kombe la Shirikisho mechi itakayopigwa uwanja wa Lake Tanganyika jumamosi Machi 29 mwaka huu ambapo wanaamini ushindi watakaopata ndiyo utapeleka morali kubwa kwenye ligi ya NBC.
Kocha Salum Mayanga akizungumzia nafasi yake kwa timu ya Mashujaa alisema kuwa anafarijika kukuta timu ina vijana wenye ari ambao wako tayari kupambana na atafanya awezalo kuhakikisha timu inarudi na kufanya vizuri kwenye mechi za ligi ya NBC lakini pia mechi yao ya kombe la Shirikisho na Pamba na Jiji.
Mayanga alisema kuwa nafasi ya timu iliyopo sasa ni Dhahiri ilikuwa na ukame wa kufunga magoli hivyo ataanza na hilo kuwanua washambuliaji vilivyo lakini pia kuhakikisha nafasi ya ulinzi inakuwa imara isiweze kuruhusu mabao kirahisi ambapo alisema kuwa mchezo wa mechi ya Shirikishi na timu ya Pamba jiji itakuwa ndiyo kipimo kuelekea kwenye mafanikio ya ligi ya NBC.
Mwisho.
0 Comments