Header Ads Widget

MAELEZO KUHUSU BAADHI YA ALAMA KATIKA NOTI NA SARAFU



Kumekuwa na mijadala kuhusu alama zilizopo katika noti na sarafu za Tanzania, hususan alama ya nyoka inayoonekana kwenye noti ya shilingi 500. Benki Kuu ya Tanzania inapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:

Utengenezaji wa noti na sarafu za nchi yoyote ile huanza baada ya kukamilika kwa mchakato wa usanifu na michoro ya fedha husika.

Usanifu huo unahusu, michoro na alama mbalimbali ambazo zinaelekeana na nchi husika. 

Katika kutekeleza jukumu la kuamua nini kitumike au kisitumike katika kutengeneza fedha, nafasi ya wananchi huzingatiwa. Hapa nchini, Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu kubwa katika maamuzi hayo.


Alama za kawaida katika noti na sarafu nyingi hapa duniani ni kama picha za watu mashuhuri, picha zinazoonesha shughuli za kiuchumi, mali asili kama milima na maziwa, majengo marefu na wanyama.

Alama na michoro inayokuwa katika noti na sarafu ina maana halisi ili kuepusha tafsiri potofu ambazo zinaweza kutokea.  

Ni wajibu wa Benki Kuu ya Tanzania kuhakikisha kwamba picha, michoro na alama zozote zinazoleta ukakasi zinaepukwa.


Kiwango cha elimu na namna ya utunzaji wa pesa kinachangia namna fedha ilivyo pamoja na alama zake.

Inatakiwa namna fedha ilivyo na alama zake ziwe zinaelekeana na kuwa rahisi kuzitambua.

Hivyo, alama ya nyoka aliyejiviringisha katika fimbo ambayo inaonekana na katika noti ya shilingi 500, inamaanisha utoaji wa huduma za afya. Hii ni alama ya huduma ya tiba inayotumika karibu duniani kote, zikiwemo taasisi za afya za hapa nchini na za kimataifa. Benki Kuu ya Tanzania iliweka alama hiyo katika noti ya shilingi 500 kuonesha umuhimu ambao serikali inaweka katika huduma za afya. 

Upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, wakiwemo watoto, ni suala ambalo linapewa kipaumbele na Serikali. Hili linajidhihirisha wazi katika mgawanyo wa bajeti ya serikali ambapo sekta ya afya inapata rasimali ya kutosha.

Imetolewa na:

Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki

24 Agosti 2018,

Wasomaji wa Matukio Daima Media, Kama chombo cha habari tumerejea kupakia maudhui ya taarifa hii ili kuupa Umma taarifa juu ya suala hili ambalo limekuwa likirejea mara kwa mara kwa nyakati na vipindi tofauti.


Na Andrew Chale, Matukio Daima App,Dar Es Salaam.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI