Wanasiasa wengi wanaahidi mambo kadhaa wa kadhaa wakati wa uchaguzi kama kuboresha elimu, huduma za afya na maji, barabara na hali za kiuchumi mara tu watakapochaguliwa; wakati mwingine wanapenda kuahidi kujenga daraja hata mahali ambapo hakuna mto.
Hayo (wanayoyaahidi) yote huyaandika kwenye vipeperushi vyao, lakini hawaainishi ni namna na mbinu gani watakayotumia kuyafikia maendeleo na kutatua changamoto hizo, na ndiyo maana wanapochaguliwa tu wanasahau kila kitu walichoahidi wananchi.
Ukitaka kujua haya nisemayo, tafuta kipeperushi cha mwanasiasa ye yote, awe mbunge au diwani, angalia alichoahidi na anachofanya sasa, bila shaka yoyote utaona ni vitu viwili tofauti kabisa.
Na sababu unaweza ikawa ama hajui alichokiahidi, alikaririshwa tu na wapambe wake bila kumpa mbinu ya kuyafikia hayo anayoahidi, Au aliamua kuwahadaa na kuwadanganya wananchi kwa makusudi ilhali anajua mambo anayoyaahidi hayatekelezeki.
Hawa ndiyo huwa wanaahidi kujenga daraja hata ambapo hakuna mto, na mara nyingi wanapokuwa madarakani hasa kuelekea uchaguzi mwingine hujaribu kudhibiti watu wanaoweza kuwahoji na kuwakosoa mienendo ya uongozi wao.
Hulka nyingine waliyonayo wanasiasa wa aina hii hupenda kuhodhi madaraka ya chama, na idara nyingine za kiserikali, unakuta wao ndiyo chama na chama ndiyo wao, viongozi wa chama wanakuwa hawana nguvu yoyote ya kitendaji na wasiweze kutekeleza majukumu yao isipokuwa kwa maelekezo ya mbunge au diwani.
Haya yanafanyika maeneo mengi nchini ikiwepo hapa Nzega, yaani diwani ambaye ni mjumbe tu wa kamati ya siasa, unakuta ndiye mwenye mamlaka kwenye chama ngazi ya kata hadi matawini kuliko viongozi wa chama, anaelekeza kila kitu na anatoa amri ya hili na ile lifanyike.
Bahati mbaya viongozi wa chama ama kwa kutoyajua majukumu yao au kwa kuhodhiwa kwa mbinu mbalimbali ikiwemo ya kifedha na vitisho.
Halikadhalika Mbunge, naye vivyo hivyo kwa watendaji wa chama ngazi ya wilaya, mbaya zaidi hata kwa mkuu wa wilaya, mkurugenzi na wakuu wa idara, unakuta kahodhi madaraka yao na kutumikishwa kufanya kazi zake za kisiasa.
Yote haya ukiangalia sababu ni mtu kujiingiza kwenye majukumu ya kisiasa akiwa hayajui majukumu hayo, matokeo yake ni kwamba mbunge kutaka kufanya kila kitu na hadi muda wake unakwisha anakuwa hajafanya kila kitu.
Na kitendo cha kutaka kufanya kila kitu kinawazuia watu wengine kushiriki kuchangia maendeleo ya jamii.
Kwa mfano hapa Nzega, Mbunge amekuwa akijaribu kufanya kila kitu yeye kiasi kwamba wananchi wengine wanazuiwa kutoa mchango wao wa maendeleo ktk jamii, na hayo anayoyazuia yasifanyike akiwa anajua hana uwezo wa kuyafanya.
Jamii inakosa maendeleo kwa sababu za kisiasa, hata hivyo, sijawahi kuona kwenye kipeperushi cha mgombea ubunge pameandikwa au ameahadi kuwa atatoa pikipiki kwa viongozi wa chama wakati wa uchaguzi ujao, wala kutoa baiskeri kwa mabalozi wakati wa uchaguzi ukifika.
Yote wanayoyafanya wabunge wakati wa uchaguzi unapokaribia hayahusiani na ahadi walizoahidi wakati wanagombea huko nyuma, na hata kama ingekuwa waliahidi, haiwezekani iwe hivyo (watoe pikipiki na baskeri) wakati wa uchaguzi unapokaribia.
Hizi ni kampeni za wazi wazi wanazotumia wanasiasa kwa kutumia koti la nafasi walizonazo.
Kwa hiyo, ni muhimu ieleweke kwamba, ikiwa mbunge au diwani anafanya mambo ambayo hakuyaahidi wakati wa uchaguzi uliopita kama kutoa baiskeri, pikipiki au pesa kwa kujifichia "kutimiza ahadi" ni vema achukuliwe kama mwanachama mwingine anayefanya kampeni ya kuwashawishi wapiga kura kabla ya kampeni kuruhusiwa.
Lakini pia, kama ni ahadi, isiwe kinga ya yeye kutoa baiskeri, pikipiki au pesa wakati kama huu wa kuelekea uchaguzi, ni vema chama kiwe kinazuia mwanasiasa kuahidi jambo fulani kulitekeleza wakati au mwaka wa uchaguzi kwa sababu linalenga kuwashawishi wapiga kura.
Hoja hii ni muhimu itiliwe maanani kwa sababu inajenga matabaka na chuki, upendeleo na inawanyima haki wanachama wengine.
Mambo haya tuliyapinga na kuyapiga vita wakati nikiwa katiba Hamasa na Chipukizi UVCCM Wilaya ya Nzega 2019 - 2020, wakati Mbunge Hussein Bashe amejipa mamlaka ya Katibu wa CCM Wilaya na kutaka kwenda kutoa maelekezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa viongozi wa chama ngazi ya Kata na matawi.
Mbunge hana mamlaka yoyote ya kutoa maelekezo ya kitendaji ndani ya chama, wala hawezi kumwakilisha katibu wa chama, yeye ni mjumbe tu wa kamati ya siasa ngazi ya wilaya, halikadhalika kwa upande wa Diwani, naye hana mamlaka yoyote kwenye chama ya kitendaji kiasi cha kutoa maelekezo kwa viongozi wa chama ngazi ya kata au matawi.
Viongozi wa chama lazima walielewe hili na wasimamie misingi ya chama, misingi ya maadili na uongozi wa CCM badala ya kuwa wanapokea maelekezo kutoka kwa mbunge au diwani.
Hata huyo katibu wa chama ngazi yoyote, iwe ya tawi, kata au Wilaya, hawezi kufanya maadili binafsi kuwa ni ya chama, chama kina misingi yake ya kimaadili.
Kwa hiyo, isitokee katibu wa chama ameelekezwa na diwani au mbunge na kuyafanya kuwa ndiyo ya chama, mambo haya tuliyakataa wakati wa uongozi wetu, hatukuyapa nafasi kabisa kwa sababu yanafedhehesha chama chetu.
Mimi kama mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), siko tayari kuona chama chetu kinakufa kwa sababu ya mtu/mwanachama mmoja, au kikundi cha watu wachache, lakini zaidi siko tayari kuona taifa letu linakufa kwa sababu ya CCM.
Ikiwa mambo haya ya kipumbavu yanaendelea ndani ya CCM ktk Wilaya yetu ya Nzega, na ye yote mwenye mapenzi mema na chama chetu na taifa letu, nawasihi msimamie misingi ya chama, muwe imara kupiga vita mambo haya yakipumbavu yanayofanywa na wanasiasa au viongozi wasio na mapenzi mema na chama chetu na taifa letu kwa ujumla, ukishindwa hili toa taarifa kwa viongozi wa chama na fuatilia wanavyolishughulikia, ukishindwa hilo toa taarifa kupitia namba hii.. 0784977072 Kwiyeya Singu.
0 Comments