Na Gabriel Kilamlya Habari na Matukio APP NJOMBE
Imeelezwa kuwa Changamoto lukuki zinazolikabili Taifa la Tanzania na Wananchi wake kutokana na uzembe wa kufikiri kwa viongozi Wengi kumetajwa kukifanya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kutaka mabadiliko ya katiba na mifumo mbalimbali.
Katika mkutano wa Hadhara wa Chadema mkoani Njombe Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa John Heche amesema kwa Rasilimali zilizopo katika nchi hii Taifa halihitaji kuendelea kutegemea misaada toka mataifa mengine bali uzembe wa kufikiri kwa baadhi ya viongozi kunasababisha Taifa kuendelea kuwa tegemezi.
Aidha Heche amesema wingi wa rasilima zilizopo katika Taifa hili zingesimamiwa vizuri Zinaweza kuwalipa shilingi milioni Moja kila mwezi Mwananchi asiye na kazi.
Akizungumza katika mkutano huo aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema Taifa Dokta Wilbroad Slaa amelitaka jeshi la Polisi kuzitii Sheria na sio kuzikiuka kwa kuwazuia vyama vyama upinzani kufanya Mikutano ya kisheria kama walivyofanya wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Elizabeth Mamboso katibu wa Chadema Wilaya ya Ilala Dar es Salaam anasema hawako Tayari kuhalalisha uchaguzi ujao bila mabadiliko ya katiba na Tume huru ya uchaguzi.
Katibu wa Chadema mkoa wa Njombe Baraka Kivambe anasema wanapaswa kuendelea kupaza sauti ili kuwasaidia wananchi kwani hata miundombinu ya barabara hususani barabara ya kwenda Lupembe inayoingiza mapato mengi haijalimwa kwa kiwango Cha lami kwa miaka yote.
Patrick Ole Sosopi Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la vijana Chadema Taifa anasema rasilimali za nchi zinapaswa kulindwa na kila mtanzania kwa kukubali kufanya mabadiliko ya kisheria na katiba.
Mjumbe wa kamati kuu ya Chadema Taifa Rose Mayemba amewatupia lawama Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Njombe kuhangaika kubadili jina la Jimbo la Njombe Mjini wakiamini Maendeleo yatapatikana badala ya kutumia akili kuleta Maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la vijana Chadema Taifa BAVICHA Deogratias Mahinyila anasema Polisi hawana Mamlaka ya kuwaandikia vibali Chadema vya kuwaruhusu kufanya au kutofanya Mikutano ya hadhara kwani Sheria haijasema Polisi wajibu Vibali vya Mikutano.
0 Comments