Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MEYA wa manispaa ya Kigoma Ujiji Baraka Lupoli amemuangukia na kumuomba radhi Waziri wa nchi ofi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) kwa maneno waliyotoa madiwani wajumbe wa kamati ya fedha na uongozi wa manispaa hiyo ambao aliwaongoza kutembelea miradi ya TACTIC inayotekelezwa kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya dunia.
Akizungumza katika baraza la madiwani la Manispaa ya Kigoma Ujiji lililokuwa likipokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi ya halmashauri hiyo ya kipindi cha robo mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana Meya huyo wa manispaa ya Kigoma Ujiji alisema haikuwa dhamira yao kutoa maneno ya kumkwaza kiongozi huyo wala wataalam wowote wa TAMISEMI wala serikali.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Februari 6 mwaka huu kamati hiyo ya fedha na uongozi ikiongoza na Meya Lupoli ilitembelea miradi ya ujenzi wa masoko ya Mwanga na Katonga, mradi wa barabara ya kiwango cha Lami kutoka Bangwe hadi Ujiji na ujenzi wa daraja la Mto Luiche.
Meya Lupoli anakiri kuwa wakati wa ziara hiyo madiwani Pamoja na yeye walitoa maneno makali kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuonyesha kukerwa kwao na miradi kuchelewa ambako kumekuwa na athari kubwa kwa wananchi ikiwemo miradi ya masoko ambapo wananchi wamehamishwa katika maeneo ya biashara lakini miradi haianzi hivyo kuwaumiza wananchi hao.
“Mimi na madiwani tulikuwa na jazba kubwa kulingana na taarifa za utekelezaji miradi tulizopata hivyo kuna maneno makali tulitoa kwa wakandarasi na TAMISEMI kuonyesha kulikuwa na ubabaishaji katika kuwapata wakandarasi hao, hata hivyo kumekuwa na tafsiri potofu kwamba tumemlenga Waziri Mchengerwa na kutaka achunguzwe jambo ambalo siyo kweli na tunamuomba radhi kwa usumbufu wowote alioupata,”Alisema Meya huyo wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Pamoja na hilo alisema kuwa walikusudia kuingiza ajenda ya azimio la kuchukua hatua kwa wakandarasi hao lakini imethibitika kwamba tayari wakandarasi wote wapo eneo la utekelezaji wa miradi hivyo azimio hilo kuliondoa na kuwaomba radhi pia Mkuu wa mkoa Kigoma na CCM Kigoma kwa namna ambavyo maneno ya madiwani hao yaliwagusa kukiwa na mijadala kwenye makundi ya mitandao ya kijamii na vijiwe mbalimbali mkoani humo.
0 Comments