Header Ads Widget

HUDUMA OFISI ZA SERIKALI YA KIJIJI, MTAA MWANANCHI LAZIMA AWE NA ANWANI ZA MAKAZI

Na Hamida Ramadhan Matukio App Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wananchi wote kutambua kwamba, ili kuweza kupata huduma ya barua ya utambulisho katika Ofisi ya Serikali ya Kijiji, Mtaa mwananchi anapaswa awe na anwani ya makazi iliyosajiliwa kwenye Mfumo wa NaPA.

Ameyasema hayo leo February 8,2025 jijini Dodoma katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya Anwani za makazi

Amesema Katika kipindi cha majaribio, jumla ya maombi ya barua za utambulisho yaliyowasilishwa ni 2,039. Kati ya hayo, maombi 1,427 sawa na asilimia 71 yaliombwa katika mitaa/vijiji tisa vya Tanzania Bara wakati maombi 612 sawa na asilimia 29 yaliombwa katika shehia nne za Zanzibar. 

"Hatua hii iliyofikiwa na nchi katika utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi ni ya kujivunia kwani hata nchi jirani ikiwemo za Uganda, Comorro na Eswatini zinaleta wataalamu kujifunza uzoefu wa Tanzania katika eneo hili. Hii, ni fursa kwa wataalamu wa ndani kutumika kueneza uzoefu kwa mataifa mengine, " Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.   

Aidha amesema Utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi ni endelevu kwa sababu ya mabadiliko ya makazi na huduma. 

"Hivyo, ushirikiano unahitajika kati ya serikali na wananchi ili kuuendeleza na kuifanya nchi yetu iendelee kunufaika na fursa za mfumo, " Amesema

Hata hivyo alielekeza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ikamilishe maandalizi ya Sheria ya Anwani za Makazi.

 Aidha, sheria hiyo iweke  sharti la msingi la kutumia anwani ya makazi katika kutoa na kupokea huduma hususan huduma zinazohitaji kutambulisha anwani husika.

Ameelekeza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ihakikishe maadhimisho haya yanakuwa endelevu na kufanyika kila mwaka pamoja na kuwa na hadhi ya Kimataifa ikiwemo kualika nchi nyingine kuja kushiriki maadhimisho hayo. 

Amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine iratibu upatikanaji wa vishikwambi kwa watendaji wa Kata, Mitaa, Vijiji na Shehia ili kurahisisha utendaji kazi katika ngazi hizo.

Ameitaka Ofisi ya Rais - TAMISEMI isimamie utekelezaji na matumizi ya mfumo wa anwani za makazi katika ngazi za Mikoa na Halmashauri  ikiwemo kuteua Waratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi na kuwapa mafunzo ya uratibu wa mfumo huo.

Pia amezitaka Halmashauri zote zitoe maelekezo pamoja na kuwasimamia watendaji wa mitaa na vijiji katika kusimamia utekelezaji, uendelezaji na matumizi ya mfumo katika maeneo yao. Watendaji pia watekeleze jukumu la kusajili, kuhakiki na kuboresha taarifa za anwani za makazi.

Ameitaka Wizara ya Fedha ishirikiane na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuboresha mfumo wa NaPA kwa kuongeza moduli itakayokuwa inasimamia vyombo vya moto.

Ameelezeka Wizara za Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zishirikiane kuhakikisha kuwa magari ya Serikali yanafungwa mfumo wa NaPA na kuhamasisha watoa huduma za usafirishaji kutoka sekta binafsi kufunga mfumo huo kwa ajili ya kurahisisha utambuzi wa maeneo mbalimbali nchini.

"TANROADS, TARURA, ZANROADS pamoja na halmashauri zote kuhakikisha zinaweka miundombinu ya anwani za makazi kwenye mitaa/barabara ambazo wana dhamana ya kuzihudumia, " Amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry Silaa amesema Maadhimisho ya Wiki ya Anuani za Makazi yana kauli mbiu ya “Tambua na Tumia Anwani yako ya Makazi Kurahisisha Utoaji na Upokeaji wa Huduma”. 

Amesema lengo kuu la Wiki hii ni kujenga hamasa kwa taasisi na wananchi kufahamu na kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi katika shughuli za kijamii na kiuchumi. 

" Katika wiki hii Shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo kutoa mafunzo maalum kwa wanachuo wa baadhi ya Vyuo vilivyopo Dodoma pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu mfumo wa anwani za makazi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii pamoja na kutembelea maeneo yenye mikusanyiko, "amesema.

#Wizara inaendelea kusimamia na kuendeleza miundombinu na mifumo ya msingi ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa kidijitali ulioainishwa katika Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Miaka 10 (2024–2034) ikiwemo mifumo ya utambuzi wa watu, biashara, ardhi, na makazi. 

Amesema Wizara imeandaa mpango wa miaka miwili utakaohakikisha waratibu na watendaji wote wapatao 21,487 wa Mikoa na Halmashauri zote za Tanzania Bara na Zanzibar wanapatiwa vishikwambi kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji, uendelezaji na matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi ambapo Vishikwambi vitabeba mifumo mbalimbali ya kidijitali ukiwemo Mfumo NIDA na RITA.

Naye Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Kufuatia maono ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa mnamo mwaka 2022 kuhusiana na kutekeleza mpango wa anuani za makazi pamoja na usimamizi wa zoezi kupitia Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, leo tunajivunia kuwa katika kila kona ya nchi hii kuna anuani za makazi.

"Ilikuwa ni ngumu kufika sehemu mbalimbali za ndani ya nchi, baada ya utekelezaji wa mpango huu, barabara na vijiji vyote vina vibao vinavyoelekeza. TAMISEMI ni wanafaika wakubwa wa mfumo huu, " Amesema

Naibu Waziri wa Ulinzi, Mawasiliano na Uchukuzi - Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Nadir Abdulatiff Alwady amesema suala la anuani za makazi kwa upande wa Zanzibar, linasimamiwa kwa umakini wa haki ya juu kwani bila kutambua wananchi wetu, hatutaweza kufikisha huduma zinazohitajika.

"Zoezi la uhakiki wa anuani za makazi kwa Zanzibar limekamilika kwa asilimia 100 katika halmashauri zote 11, pia tumejenga uwezo wa uratibu wa anuani za makani, " Amesema

Amesema Kabla ya zoezi la uhakiki, Zanzibar ilikuwa na anuani za makazi 440,124  baada ya zoezi la operesheni ya anuani hizo, Zanzibar ina jumla ya anuani 533,386.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI