Ameandika Kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye pia ni mtunzi na Mwandishi wa Vitabu vya Ujasusi nchini, Yericko Nyerere baada ya uchaguzi wa Chama hicho hivi karibuni uliopelekea Tundu Lissu kushinda nafasi ya Uenyekiti kwa kura zaidi ya 500 dhidi ya mpinzani wake aliyepata kura zaidi ya 400.
Yericko Nyerere Ameandika:
"Uchaguzi umeisha, demokrasia imeshinda! Nafanya maachilio mema kutambua na kuthamini demokrasia ya kisiasa hasa katika ardhi ya ubwa. Nilisimama wima kumuonga mkono Mh Mbowe, tumeshindwa katika sanduku la kura kidemokrasia kabisa, Kwamsingi huohuo wa kidemokrasia ya siasa za vyama, Ninapongeza uongozi mpya chini ya Mwenyekiti Mh Tundu Lissu kwasababu umepatikana kwa njia ya kidemokrasia ya haki, uwazi na ukweli. Ndio demokrasia ina pande mbili, upande wa furaha na upande wa huzuni, muda wa huzuni umeisha sasa ni muda wa ushindi wa taasisi yetu.
Lakini, Niseme nini juu ya Mtu huyu Mh Freeman Mbowe? Hakika nitaandika kurasa milioni na bado sitamaliza kumuelezea na kumheshimisha. Wewe ni Kiongozi, Wewe ni Mwalimu, Wewe ni Baba, Wewe ni Kaka, Wewe ni Rafiki na wewe ni alama ya makuzi mema. Umejenga taasisi imara ya kidemokrasia, umeiishi demokrasia, na umeiishi kwa vitendo halisi kwa kuchagua kuwa ndio mlango wetu imara wa kuingia na kutokea!
Nimejiuliza sana, mimi moyo kama wako huo Mh Freeman Mbowe nitautoa wapi? Umedhalilishwa vya kutosha, Umetwezwa vya kutosha lakini ulitakaa kujibu udhalili huo na ulitukataza tusijibu kwa moto japo tuliumia, walau tukajibu kidogo kwa moshi, umesalitiwa na watu wako wa karibu hata tulipokwambia juu ya hili ulisema wazi acheni demokrasia iamue na kweli demkrasia imeamua! Ni nani mwenye moyo kama wako Mh Freeman Mbowe katika siasa za Afrika akaruhusu haya na akasimama na kuwashukuru makutano? Hakika sijamuona na sitamuona kwa karne zijazo.
Nitakukumbuka sana katika uongozi wako, ulitetea aseti za chama kwa nguvu kubwa, mfano hai ni pale mimi nilipovamiwa nyumbani kwangu Mbutu Kigamboni kwajaribio la kutekwa kwa mara ya kwanza wakafeli, ulisimama na mimi ukasaidia mapambano nisikamatwe kwa muda wa siku 60 za kuwindana usiku na mchana katika mikoa karibu yote Tanzania nilikokuwa nakimbilia, na baada ya hizo siku 60 nilitekwa pale Shoppers Plaza Mikocheni na kisha kufunguliwa kesi nane katika Mahakama ya Kisutu na Mahakama Kuu katika kipindi cha utawala awamu ya tano.
Ni wewe Mwenyekiti wa chama uliagiza mawakili 20 wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama sasa Mh Tundu Lissu na Mh Kibatala wakaongoza jopo hilo kwa miaka 7 mfululizo hadi nikashinda kesi 7 na moja kufungwa nikaenda kushindia kule Mahakama Mkuu. Ulikuwa moyo wa kipekee sana nilitambua na kuona unavyothamini aseti za chama, mimi mwanachama wa kawaida kupewa usaidizi mkubwa vile wa kisheria kwa miaka 7 mfululizo lilikuwa tukio kuu la kiuongozi. Niseme nini sasa? Naamini hujaondoka katika siasa bali unapumzika, tutakuhitaji mapema muda ukifika.
Uchaguzi umepita, Washindi wamepatikana, Chama kimeshinda, Tunalo jukumu moja tu kwasasa nalo ni kuwaunganisha Wanachadema, Binafsi nasimama kwenye ushauri wako Mh Freeman Mbowe kwa uongozi mpya wa Mwenyekiti Mh Tundu Lissu uliposema kwamba uongozi mpya uponye majereha, na kwamba uchaguzi huu umetuacha na majeraha makubwa hili hatupaswi kulipuuza kabisa.
Jambo lingine muhimu ni kwamba Uongozi mpya usimamie kwa nguvu kubwa maazimio ya Chama kwamba Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi mkuu wa taifa (no reform no election), na hapa niseme wazi ninahimiza hizi reforms kwanza kwa haraka kwakuwa muda tulionao kuelekea uchaguzi mkuu ni mdogo sana. Lakini lililo la muhimu ni reform hizi ziende sambamba na chama chetu kujiandaa katika uchaguzi wa mwezi October 2025.
Itakuwa kosa la kimkakati na angamizo la chama chetu tukishindwa kupata reform hizo na tukashindwa kushiriki Uchaguzi huu kwani tutatimiza miaka 10 chama bila kushiriki uchaguzi na tutaruhusu chama kuondoka kwenye uongozi wa upinza na mbio za kushika dola lakini kubwa zaidi tutapoteza hata ruzuku tunayopata sasa ya 107M na mwisho uongozi mpya utakuwa umewaangusha wanachama walioahidiwa katika sera za Mh Lissu kwenye Uchaguzi kuwa katika uongozi wake ruzuku itaanza kushuka mikoani, wilayani majimboni, katani na katika mitaa/vijiji." Yericko Nyerere.
0 Comments