Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Jumla ya watu 775.119 wamefikiwa na mpango wa kampeni ya usaidizi wa kisheria bila malipo kupitia mpango wa Usaidizi wa kisheria wa Mama Samia ambao kwa sasa mikoa 11 nchini imetekeleza mpango huo.
Waziri wa Katiba na Sheria,Dk.Damas Ndumbaro alisema hayo akizindua mpango huo kwa mkoa Kigoma ambao kwa sasa unakuwa mkoa wa 12 nchini kutekeleza mpango huo ambapo amebainisha kuwa hadi sasa jumla ya mashauri 3162 yamepokewa na wanasheria na kupatiwa ufumbuzi.
Akieleza maendeleo ya kampeni hiyo Waziri Ndumbaro alisema kuwa katika mikoa 11 ambayo mpango huo umetekelezwa mashauri makubwa yaliyojitokeza ni Pamoja na migogoro ya masuala ya ardhi, masuala ya ukatili kwa wanawake na Watoto, masuala ya mirathi na ndoa na kwa mkoa Kigoma limeibuka suala la matatizo ya uraia ambalo watalichukua na kuendelea nalo kwa mikoa yote iliyobaki nchini
Awali Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia, Watoto, wazee na makundi maalum, Amon Mpanju alisema kuwa mpango huo umekuja wakati muafaka na hasa kwa wizara hiyo ambayo watu wake wanawake na Watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa masuala ya migogoro mbalimbali inayojitokeza.Naye Mkuu wa wilaya Kigoma,Dk.Rashidi Chuachua akitoa salamu za mkoa kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa kampeni hiyo itakuwa chachu ya maendeleo kwa mkoa kutokana na kuondoa migogoro iliyokuwepo na haki zao kusimamiwa kikamilifu na kwamba wananchi wa mkoa huo wapo tayari kupokea huduma hiyo.
0 Comments