Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu nchini kutumia elimu yao katika kukuza uchumi wa nchi na kutumia tafiti wanazofanya ziweze kusaidia katika Maisha ya kawaida ya wananchi.
Majaliwa alisema hayo mkoani Kigoma katika mahafali ya 43 ya Chuo Kikuu huria ambapo wahitimu 4307 wamemaliza kozi mbalimbali wakiwemo wahitimu 55 ambao wamemaliza Shahada ya Uzamivu wa Udaktari wa Falsa (PHD) miongoni mwao wakiwemo wanawake 20.
Waziri Mkuu alisema kuwa taasisi za elimu ya juu zinalo jukumu kubwa la kutoa wataalam ambao ndiyo nyenzo kuu katika kuendesha shughuli mbalimbali za serikali kwa utaalam wao na ndiyo maana serikali imeamua kwa dhati kabisa kuwekeza katika kuhakikisha vyuo vya elimu ya juu vinatoa wahitimu wenye utaalam wa kutosha katika Nyanja mbalimbali.
Alisema kuwa Tanzania kwa sasa imeweka mkakati wa kuwa nchi ya viwanda hivyo ni jambo lisilowezekana kuzungumzia viwanda bila kuzungumzia wataalam ambao watasimamia uendeshaji wa viwand hivyo.
Akieleza umuhimu wa chuo kikuu huria alisema kuwa kimekuwa moja ya nyenzo muhimu za kutoa elimu kwa kuwapa nafasi nzuri wananchi kupata elimu yao popote walipo bila kuathiri shughuli zao za kiuchumi za Maisha hivyo ametoa wito watu wengi Zaidi kutumia chuo kikuu huria kusoma na kupata utaalam kwani elimu inayotolewa na sawa na vyuo vingine nchini.
Sambamba na hilo Waziri Mkuu Majaliwa amezitaka taasisi za elimu ya juu kuweka mkazo kwenye masuala ya ubunifu na bunifu zinazofanywa na wahitimu wa vyuo ziweze na tija kwa maendeleo ya nchi akita pia hivyo kazi za ubunifu kuuzwa kwa wenye mahitaji kwani kwa sasa kazi za ubunifu zimekuwa biashara.
Akitoa salam katika mahafali hayo Mwenyekiti wa baraza chuo kikuu huria, Profesa Joseph Kuzilwa ameishukuru serikali kwa kuweka mazingira mazuri ambayo yanahakikisha shughuli za kutoa elimu kwa njia ya masafa haikwami na hivyo kuweza kuongeza idadi ya wanafunzi kila mwaka.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya chuo hicho Makamu Mkuu wa chuo Kikuu huria, Profesa Elifasi Bisanda alisema kuwa mahafali hayo ya 43 yanaadhimidha pia miaka 30 ya kuanzishwa kwa chuo hicho.
0 Comments