-Chongolo aonya polisi kuchepusha ushahidi.
Na Moses Ng'wat, Ileje.
WITO umetolewa kwa wazazi na walezi Mkoani Songwe kuwa mstari wa Mbele kutoa ushirikiano wa kutosha dhidi ya matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto yanayoripotiwa polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa kitengo cha Dawati la jinsia kutoka jeshi la polisi Mkoa wa Songwe, Mkaguzi Msaidizi wa polisi, Eletisia Mtweve, katika maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Ileje leo Disemba 10 2024.
Mtweve, amesema dawati la polisi la jinsia licha ya kupokea taarifa ya vitendo vya ukatili lakini lakini hushidwa kuendelea na michakato ya kisheria ili haki kutendeka kwa kuwa hukwamishwa na baadhi ya wazazi na walezi, ikiwemo jamii kushindwa kutoa ushirikiano iliwemo kumalizana nyumbani.
Amesema katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia , dawati limeadhimisha siku hizo kwa kutoa elimu maeneo mbalimbali pamoja na kupokea wateja (Wahanga) 41 ambapo wakike ni 36 na wanaume watano.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Frida Mgomi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa Songwe, Daniel Chongolo, katika maadhimisho hayo, alitumia jukwaa hilo kutoa wito kwa kila mtu kujitathmini majukumu yake na kwa nafasi
yake aliyonayo katika Jamii katika mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
"Ndugu Wananchi,kama tunavyofahamu mkoa wetu ni moja ya mikoa yenye ukatili mwingi wa kijinsia, ikiwemo mimba zautotoni na ndiyo inayoongoza kwa kuwa na changamoto kubwa ya mimba kwa asilimia 45" amesema Mgomi.
Amesema Mkoa huo umeendelea kutoa elimu ya Ukatili na madhara yake kwa Jamii, kupitia Wataalamu mbalimbali wakiwemo Maafisa Ustawi wa
Jamii, Polisi Dawati, Wanasheria, Maafisa Maendeleo wa Jamii,
Madaktari na Wauguzi, na Wadau mbalimbali ambao wamekuwa
wakikutana na kuwahudumia Wahanga wakubwa katika huduma mbalimbali ambao ni Wanawake na Wanaume, Wasichana na Wavulana.
Hata hivyo, ametaka wahanga wa matukio ya ukatili kutoa taarifa ndani ya maasa 72 wa uwepo wa kiashirikia au
matendo ya ukatili miongoni mwao katika ngazi zote za Halmashauri, kata, vijiji na Vitongoji.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa aliotoa onyo kwa jeshi la polisi juu ya malalamiko ya kuchepusha ushahidi kwenye kesi za matukio ya ukatili wa kijinsia kama kulawiti na ubakaji, ikiwemo kuchukua rushwa.
Malalamiko ya polisi kushindwa kutenda haki kwenye upelele kwa kuchepusha ushahidi, ikiwemo vyombo vya sheria kushindwa kutenda haki kwenye matukio ya ukatili wa kijinsia kama ulawiti na ubakaji yaliibuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Radiwello Mwampashi, wakati akitoa salama za chama katika maadhimisho hayo.
Akizungumza kando ya mkutano huo wa maadhimisho, mmoja wa wakazi wa Isongole,Maria Kibona, amesema wanashindwa kuripoti matukio ya ukatili kutokana na vitisho wanavyopewa dhidi ya wananchi kwani baadhi yao hutenda makosa hayo kutokana na Imani za kishirikina.
"Matukio ya ubakaji ,ulawiti yapo lakini tunaogopa kuripoti kwani tunahofia maisha ,lakini elimu tuliyoipata Leo kwenye maadhimisho haya tutakuwa msitari wa mbele kuripoti ili wahusika washughulikiwe," amesema Kibona.
0 Comments