Header Ads Widget

WATALII ZAIDI YA 5000 WAMEFIKA MISITU YA MAGAMBA WILAYANI LUSHOTO MKOANI TANGA KUJIONEA VIVUTIO VYA UTALII

Mhifadhi mkuu wa Wakala wa misitu TFS Hifadhi ya Magamba wilayani Lushoto mkoani Tanga Christoganus Vyakuta amesema kutokana na filamu ya Royal tour aliyotengeneza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wilayani Lushoto kumekuwa na ongezeko la watalii wa nje na wa ndani ambapo hadi kufikia Novemba mwaka huu zaidi ya Watalii 5000 wamefika kujionea vivutio vya utalii wilayani humo.

Hayo yamesemwa na Mhifadhi mkuu was Wakala wa misitu TFS Hifadhi ya Magamba wilayani Lushoto mkoani Tanga Christoganus Vyakuta wakati akizungumzia vivutio vya utalii vilivyomo katika misitu ya Magamba ambako siku ya tarehe 7 mwezi huu kutakuwa na hafla ya matembezi ya watalii katika misitu hiyo.

Amesema katika Lushoto kuna kila kitu kinachohusu utalii ikiwa ni pamoja na kivutio cha hali ya hewa ya ubaridi tofauti na maeneo mengine ya nchi yetu.

''Lushoto kuna hali ya hewa ya baridi ambayo imekuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii wengi hasa kutoka nje ya nchi'' alisema Vyakuta. 

Alisema kuna siri kubwa sana katika kutembelea utalii wa kimazingira kwani uhimarisha afya ya Mtalii hasa kutokana na hali ya hewa nzuri ya wilaya hiyo.

Alisema hasa Wajerumani wamekuwa wakifika katika wilayani hiyo kujionea kumbukumbu mbali mbali za wajerumani zilizoanzishwa hapa nchini kipindi cha ukoloni.

Naye Afisa Utalii wilaya ya Lushoto Shadrack Makaya amesema maeneo ya Usambala yamekuwa ni chachu kubwa ya Utalii hasa kutokana na vivutio vya kiasili ambapo katika milima ya usambala kumekuwa na njia za kutembea kwa miguu ambazo huvutia watalii.

Alisema pia watu hawajui kuwa hali ya hewa ya baridi nayo ni kivutio kikubwa kwa watalii ikiwa ni pamoja na mapolomoko ya maji yapo sehemu nyingi ambayo yamekuwa ni kivutio pia.

''Kuna watu hawafahamu kuwa kuna Utalii baridi ambao kumekuwa ukileta watalii wengi sana huku Lushoto tofauti na maeneo mengine hivyo sasa hivi tumeandaa mikakati kikubwa ya kuweza kuhamasisha watu wengi waje huku kwani huku muda wore ni baridi kabisa'' alisema Makaya.

Alisema Lushoto kuna mapango ya kihistoria ya aina mbali mbali wakiwemo viumbe hai walio katika misitu ya milima ya Usambala na kuvutia wageni.

''Pia Lushoto tuna mawanda ya uono wa juu na chini nyingi sana ambayo ukizunguka pembezoni mwa milima hii utaona uono mbali mbali kama uwanda wa Ilenje, uwanda wa Mambo ambao ukiwa pale juu unaweza kuona mlima Kilimanjaro vizuri hasa wakati wa asubuhi pamoja na kuona hifadhi ya Mkomazi kwa juu na kuona sehemu ya misitu ya hifadhi ya Tsavo nchini Kenya ukiwa katika uwanda wa juu wa Mambo'' alisema Makaya.

Alisema pia wilayani Lushoto kuna majengo ya Kihistoria ambayo yaliachwa na Wajerumani  ni vivutio kikubwa kwa watalii ''Ukiangalia hapa Lushoto utaona majengo mengi ya asili ya kijerumani na kuna mitaa ina majina kama yaliyopo huko ujerumani kama mtaa wa Dochi ambao jina uliitwa na Wajerumani''

''Wengine hawajui kuwa Wilayani Lushoto kuna kituo cha kwanza cha Polisi ambapo hapa ndio Jeshi la Polisi lilipoanzia kwa kuanzishwa na mkoloni na kuna Ikulu kongwe ipo hapa ambayo inaweza kuwa kongwe kwa Afrika Mashariki kwasababu ilitengenezwa na wakoloni pamoja na ofisi ya Gavana ambayo inatumika na Mkuu wa wilaya na Maeneo mengine maalufu ambayo tunaendelea kutunza kwaajili ya kumbukumbu''

''Pia tunaendelea kutunza mila na desturi za kihistoria za makabila ya wazawa kama wasambaa, wadigo, wapare, wambugu, wazigua na wamasai kwani  makabila hayo yalikuwa yakikaa huku ikiwa ni pamoja na kuendelea kutunza historia ya Chifu Kimweri ambaye alikuwa maalufu hivyo tunatunza ii vizazi na vizazi waendelee kujifunza wamfahamu''  alisema Makaya.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI