VIJANA Wilayani Kibaha wametaka sheria ya kazi ibadilishwe ili watumishi wastaafu wakiwa na miaka 50 badala ya 60 ili kutoa nafasi ya ajira kwa vijana kupunguza changomoto ya ajira.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Omary Punzi ambaye ni mratibu wa kongamano la kujadili sera ya taifa ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2007 toleo 2024 na mikakati ya kupunguza umaskini.
Punzi amesema kuwa moja ya hoja ambayo ilitajwa sana na vijana ni kuhusiana na suala la ajira ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa vijana nchini.
Naye katibu wa makongamano hayo Hendrika Laurent amesema kuwa baadhi ya vijana wengi hawajui sera ya maendeleo ya vijana na dhima haiendani na dira ya sera inasababisha vijana kutofikia dira na kutojua malengo ili kujikwamua.
Naye Beth Msimbe kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Pwani amesema kuwa vijana wanapaswa kujiwekea fedha kwa ajili ya maisha yao ya baadaye pamoja na matibabu pale wanapopata changamoto za kiafya.
Ofisa Masoko wa UTT-AMIS Dorice Mlenge akizungumzia masuala ya uwekezaji amesema kuwa wananchi wanapaswa kuwekeza kwenye mfuko huo ili wajipatie fedha na dhana ya uwekezaji ina faida kubwa pia ni faida kwa maisha yote na kwa watoto hivyo wawe na mtazamo wa kujiwekea akiba ambayo itawasaidia baadaye.
Moja ya washiriki Diana Gregory alisema kuwa kuhusu suala la umri wa kazi ni vema likaangaliwa upya kwani linawakwamisha vijana kuajiriwa pia watumishi hao wanapostaafu wanakuwa hawana uwezo tena wa kufanya kazi.
0 Comments