Na Moses Ng'wat, Songwe
MKOA wa Songwe unatarajia kuzindua kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campain-MSLAC), Disemba 12 mwaka huu, katika viwanja vya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mjini Vwawa, Wilayani Mbozi.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo Disemba 11, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amesema mara baada ya uzinduzi, kampeni hiyo inatarajia kufanyika kwa siku tisa ambapo wananchi katika maeneo yao wataendelea kupata huduma za msaada wa kisheria.
Hata hivyo, amesema kampeni hiyo inatarajia kufanyika katika Halmashauri zote tano za Mkoa wa Songwe, ambapo kila Halmashauri itafanyika kampeni hiyo ya huduma za kisheria katika kata kumi.
"Napenda kuwasihi wananchi wa Mkoa wa Songwe kujiandaa na baadae kujitokeza kwa wingi wakati wa kampeni hii inayotarajia kufanyika kwa siku tisa na pia kuhakikisha wanatumia fursa hii adhimu kuwasilisha changamoto zote za kisheria zinazowakabili" alisisitiza Dc Mgomi.
Vile vile, Magomi amesema kampeni hiyo inalenga kutoa huduma za kisheria bure na inatarajia kuzingatia maeneo muhimu ikiwemo msaada wa kisheria kwa waathirika wa vitendo vya unyanyasaji, kutetea mageuzi ya kisera ili kukuza usawa wa kijinsia na haki za kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Richard Kilanga, ameitaja Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kuwa inalenga kutoa fursa kwa wale wote ambao wamenyimwa haki zao na kuwapa uwezo wa kudhibiti maisha yao.
Kilanga amesema jumla ya wataalamu wa kisheria 50 watakuwa wametapaa katika Halmashauri zote za Mkoa wa Songwe kwa ajili ya kutoa huduma za kisheria katika siku zote tisa za kampeni hiyo.
x
0 Comments