Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Godfrey Chongolo, Disemba 19, 2024 amefikiwa na Mkurugenzi wa idara ya mambo ya ndani ya mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ndositwe Haonga, ofisini kwake huko Selewa Vwawa mkoani humo.
Akizungumza mkoani humo, Kiongozi huyo kutoka TRA, amesema ziara hiyo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa inayolenga kuwashukuru walipakodi kwa mchango wao mkubwa katika mapato ya Serikali katika ukusanyaji wa kodi.
Katika kampeni hiyo, walipakodi wa makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo wanapewa shukrani kwa njia ya zawadi ili kutambua mchango wao katika ujenzi wa Taifa kupitia kodi wanazolipia kwenye biashara zao.
Hata hivyo hatua hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na wadau wake, wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa serikali na ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Songwe, katika juhudi za kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafanikiwa.
Akizungumza na ujumbe huo, mkuu wa mkoa wa Songwe Mhe. Chongolo amepongeza hatua ya TRA kuwakumbuka na kuwashukuru wateja wao akisema ni kitendo cha kuimarisha uhusiano wa karibu, jambo ambalo pia linasaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya ukusanyaji wa mapato.
Aidha, Chongolo amempongeza Kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda kwa kazi nzuri anayodai imekuwa ikifanyika kwa ufanisi.
0 Comments