Na Lubango Mleka, Igunga.
WAKULIMA wa zao la Pamba Wilaya ya Igunga Mkoni Tabora wametakiwa kulinda hadhi ya Wilaya hiyo kwa kuzalisha mbegu bora za zao hilo na kutakiwa kuazimia kushika nafasi ya kwanza kwa uzalishaji wa zao la Pamba nchini.
Aidha, wametakiwa kung'oa maotea yote ya zao hilo na kuyachoma moto kabla ya kuanza msimu mpya wa kilimo inaotarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kufanya hivyo kutawaletea tija na faida lukuki zitakazo wainua kiuchumi.
Hayo, ameyasema leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha wakati akizungumza na Wakulima wa zao hilo katika vijiji vya Mwabakima, Mwamashimba na Jogoya vilivyopo wilaya ya Igunga mkoani Tabora, ambapo amewataka wale ambao bado hawajang'oa maotea hayo wang'oe mara moja kabla ya mkono wa sheria haujawafikia.
Aidha, amewaagiza Maofisa Tarafa, Watendaji Kata na Kijiji kufanya msakao na kuchukua hatua kwa atakayekutwa amekaidi agizo hilo mara moja baada ya muda alioutoa kutekeleza agizo lake kumalizika.
"Ninawasihi kila mmoja ashike nafasi yake, mkae katika viti vyenu sawasawa, fanyeni kazi zenu hali yakuwa mmetulia panapostahiki kuchukua hatua kwa kufuata haki chukueni hatua za haraka, "
"Mtendaji wa Kata na Ofisa Ugani chukueni hatua dhidi ya mtu yoyote anayesema hataki kung'oa na kuchoma maotea kwa wakati akatafute sehemu nyingine sio Igunga kwa sababu maagizo ya Serikali ni lazima yaende, " amesema Chacha.
Ameendele kusema kuwa, Wakulima hao watakuwa watu wa ajabu ikiwa kiwanda cha kutenganisha mbegu na Pamba yenyewe kilicho kusudiwa kujengwa Igunga kisijengwe kwa sababu kunawatu hawatoi masalia ya pamba, maotea na kuchanganya mazao mengine na zao hilo au kutokufuata utaratibu uliowekwa na halafu wao hawataki kufuata maelekezo.
"Ninataka mniandikie mmemkataza mkulima gani na kwamba hatakiwi kulima pamba tena hapa Igunga, halafu msimamie utekelezaji wake na kuwaandikia Bodi ya Pamba kuwa ameondolewa mpaka atakapo jirekebisha," akisema Chacha.
Ameongeza kuwa Igunga tayari inayo sifa ya kuzalisha mbegu za Pamba nchini, hivyo heshima hiyo wailinde na kuitunza kwa sababu kiwanda hicho kikijengwa watapata faida.
Chacha, mewataka Maofisa Ugani hao kuhakikisha vishikwambi walivyopewa na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wanavitumia kujaza takwimu mbalimbali za serikali ikiwemo zile za zao la pamba na mazao mengineyo.
Amesema wanatakiwa kuvitunza kama ilivyo kwa watumishi wanaoendesha magari na pikipiki kwa sababu sio mali zao ni za serikali.
"Ndugu viongozi yote hayo ni mipango ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwarahisishia watumishi wa umma majukumu yao, hivyo tuendelee kumshukuru na kumpongeza Rais wetu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya.," anasema Chacha.
Huku, Mkuu wa wilaya hiyo, Sauda Mtondoo akisema kuwa, msimu wa kilimo 2024 hadi 2025 makampuni 15 yalipewa kibali cha kununua pamba, hivyo wilaya ilifanikiwa kukusanya sh. bilioni 1.166.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya ya Igunga, Mafunda Temanya amemhakikishia Mkuu wa mkoa huo kuwa CCM itatoa maelekezo na katu haitawatetea wakulima wa namna hiyo.
Twalib Salum Ngahoma ni Ofisa kilimo kata ya Mwamashiga, akizunguza kwa niaba ya Maofisa kilimo wilaya ya Igunga, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa kilimo na viongozi wote wa mkoa wa Tabora kwa kuwakumbuka Maofisa kilimo na kuwapatia Vishikwambi kwa ajili ya kufanyia kazi katika kilimo jambo ambalo litawasaidia kutoa taarifa kwa kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa na Taifa ili kuweza kutatua changamoto za wakulima kwa wakati.
"Mkuu wa mkoa ametuelekeza kuvitumia vishikwambi kama ilivyoelekezwa na Serikali, na si kuvitumia kwa matumizi binafsi kama kupiga picha za utupu ambazo zitatuzalilisha sisi Maofisa kilimo na hata Serikali, hivyo tutumie kwa madhumuni lengwa ya kuwasaidi wakulima, " anasema Ngahoma.
Ameendele kusema kuwa, kuunganiswa huko kwa Maofisa kilimo kuanzia vijijini katani, wilayani, mkoani na Taifa ni jambo jema sana kwani mabwana shamba wa leo sio kama wa miaka mitatu au minne iliyopita, sasa wanakwenda kutoa elimu kwa wakulima juu ya kilimo cha kisasa, kupima afya ya udongo,
Matumizi bora ya viwatilifu na pembejeo za kilimo, lakini pia kama kunatatizo lolote lile Wizara ya kilimo ni rahisi kupata taarifa kwa wakati kwani vishikwambi hivyo vimeunganishwa kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa, hivyo wataona ni namna gani ya kutatua tazo au kama kuna jambo la kuongeza basi litafanywa kwa wakati sahihi.
0 Comments