Header Ads Widget

WADAU WA KILIMO NA MAZINGIRA SHIRIKIANENI NA SERIKALI KATIKA KUTEKELEZA MKAKATI WA KILIMO MSETO- MHE. KITANDULA



Na Matukio Daima App, Musoma Mara.


Wadau wa kilimo na mazingira wametakiwa kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kilimo mseto uliozinduliwa na Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 2024 huko Same, Kilimanjaro ambapo Wizara ya Maliasili ndio msimamizi wa utekelezaji wa mkakati huu.


Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa akifungua maonesho ya tisa ya kilimo mseto mwaka 2024 katika kituo cha Mafunzo ya Kilimo Mseto Bweri Mjini Musoma Mkoani Mara.


Aidha Mhe. Kitandula alisema kuwa Mkakati huo una lengo kuhamasisha kilimo mseto katika kukabiliana na mabadiliko ya nchi, lishe bora na kukuza kipato, pia unalenga ifikapo mwaka 2030 kaya milioni 15 ziwe zinatumia kilimo mseto.


“Vilevile Serikali ina mpango wa kutasfiri mkakati huu katika lugha ya Kiswahili na kuweka mkakati katika lugha rahisi ili kufikia wadau wengi. Hivyo tunawaomba wadau wote wa kilimo mseto na mazingira tusaidiane katika kukamilisha jambo hili” Alisema Kitandula.


Naibu Waziri amewataka wadau hao Kuanzisha jukwaa la kilimo mseto litakalo ratibu utekelezaji wa mkakati huu pamoja na shughuli na jitihada za wadau mbalimbali lakini pia waanzishe na kuendeleza bustani za miti zenye kuendana na kilimo mseto katika halmashauri za Wilaya.


Mhe. Kitandula ameitaka sekta binafsi kuwekeza kwenye kuongeza thamani na kujenga masoko kwa mazao yanayotokana na Kilimo mseto na Kuongeza miradi ya biashara ya kaboni kwenye maeneo ya kilimo mseto kwa kuwa itasaidia upatikanaji wa fedha za kuhifadhi mazingira na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi.


Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara katika ufunguzi wa maonesho hayo alisema kuwa uwepo wa Maenesho hayo katika wilaya ya Musoma ni darasa tosha kwa wananchi wa mkoa wa Mara kwa ajili ya kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.


Kilimo mseto kinajumuisha mbinu za kuchanganya miti na mazao ya chakula ili kuboresha uzalishaji wenye tija kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya chakula kwa sasa na kwa vizazi vijavyo. Maonesho ya Kilimo Mseto yameandaliwa na Shirika la Vi Agroforestry Tanzania.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI